CCM Yashinda Viti Vyote Udiwani Sengerema, Tarime Mjini
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda viti vyote 47 vya udiwani katika majimbo ya Sengerema na Buchosa wilayani Sengerema.
Pia, chama hicho kimeshinda uchaguzi katika kata zote nane za jimbo la Tarime Mjini katika uchaguzi uliofanyika jana.
Wakati msimamizi wa uchaguzi jimbo la Sengerema, Magesa Mafuru akisema CCM imeshinda kata zote 26 za jimbo hilo, mwenzake Crispin Luanda wa Buchosa amesema chama hicho kimetwaa kata zote 21 za halmashauri hiyo.
Wakizungunza kwa nyakati tofauti leo Oktoba 29, 2020, wasimamizi hao wamesema shughuli ya majumuisho ya kura za ubunge na urais katika majimbo hayo inaendelea.
Kwa upande wa jimbo la Tarime Mjini, msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo, Elias Ntiruhungwa amesema kuwa awali wagombea udiwani katika kata mbili katika jimbo hilo wapita bila kupingwa.
Amesema kuwa katika kura zilizopigwa jana kata zilizobaki sita CCM imeweza kushinda huku akisema kuwa matokeo ya ubunge yanatarajiwa kutangazwa muda wowote.