Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NHIF, Bernard Konga (kushoto) wakibadilishana mkataba wa uzinduzi wa Mpango wa DUNDULIZA kwa huduma za NHIF kupitia Benki ya NMB . Kulia ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NHIF, Bernard Konga (kushoto) wakisanini mkataba wa uzinduzi wa Mpango wa DUNDULIZA kwa huduma za NHIF kupitia Benki ya NMB . Kulia ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi.

=====  =======  =========

Benki ya NMB na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zimeweka historia mpya na ya aina yake nchini kwa kuanzisha utaratibu wa kipekee wa bima ya afya utakaowawezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo kiurahisi na kwa nafuu kubwa kwa kuweka akiba kidogo kidogo kulingana na vipato vyao. 

Historia hiyo iliandikwa jijini Dar es Salaam baada ya taasisi hizo mbili kuingia makubaliano ya kutekeleza mpango huo ambao unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye malengo ya taifa ya kuboresha rasilimali afya na upatikanaji wa tiba. 

Mpango huo mahsusi wa huduma ya afya kwa wote ujulikanayo kwa jina la DUNDULIZA ulizinduliwa katika hafla iliyofanyika PSSSF Complex na kuhudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa taasisi hizo mbili pamoja na wadau mbalimbali. 

Wakizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga,walisema ukubwa wa mtandao wa huduma wa benki hiyo utasaidia sana kuipeleka DUNDULIZA kwa Watanzania hasa wale wa kawaida kama wakulima na wajasiliamali. Pia walisema kuwa huduma hiyo mpya itakuwa na mchango mkubwa katika mipango ya serikali ya kuhakikisha afya bora kwa Watanzania wote kupitia bima ya afya. 

“NHIF wanapoingia makubaliano nasi, maana yake wataweza kuwafikia Watanzania wote kila pembe ya nchi hii kutokana na mtandao wetu mpana wa matawi na hata mtandao wa wakala wetu ambao ni wawakilishi katika huduma za kifedha. NMB ina matawi 227 na ipo katika kila wilaya na baadhi ya kata hapa nchini huku tukiwa na wakala wa benki (NMB Wakala) zaidi ya 7,000,” Bi Zaipuna aliongeza. 

Kuhusu DUNDULIZA, alisema ni mpango unaomwezesha mwananchi kujiwekea akiba ya fedha kidogo kidogo za michango kwa ajili bima yake ya afya na hata wategemezi kupitia Benki ya NMB. Kwa utaratibu huu, alifafanua, mtu ataweza kufanikisha kuchangia mojawapo ya vifurushi vya bima ya afya vinavyotolewa na NHIF ambavyo ni Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya. 

Kwa mujibu wa Bi. Zaipuna, Benki ya NMB imeamua kuwekeza katika mpango wa DUNDULIZA na kushirikiana na NHIF kuufanikisha kwa sababu afya bora ni mtaji kwao kama taasisi ya kifedha. Alisema upatikanaji wa tiba kwa kutumia bima ya afya badala ya akiba zilizowekwa benki ni swala la msingi si kwao tu lakini pia kwa wateja na wananchi kwa ujumla. 

“Huu ni mpango wa kwanza na wa aina yake kutokea hapa nchini na tunafurahia kuwa wa kwanza kuweka historia hii ya kushirikiana na Serikali kupitia NHIF katika kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania. Utaratibu huu pamoja na kupata bima ya afya pia unamjengea mwananchi utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kutimiza malengo mbalimbali,” Bi Zaipuna alifafanua. 

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF alisema kuwa wakati NHIF inazindua mpango wa vifurushi Novemba mwaka jana, changamoto iliyoonekana ni pamoja na uwezo wa wananchi kulipa fedha zote kwa awamu moja hatua iliyoifanya menejimenti ya mfuko huo kufungua milango na kuanza kushirikiana na wadau wa taasisi za kifedha kama Benki ya NMB ambayo ililipokea wazo la DUNDULIZA na kulifanyia kazi haraka.