HOFU inazidi kutanda juu ya kupotea na kutoonekana kwa msanii mtata wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini almaarufu kama Dudu Baya (46), ambapo bifu zake na mastaa lukuki Bongo, zimeibuliwa.


Dudu Baya ambaye hupenda kujiita Konki Master au Oil Chafu, amekuwa haonekani maskani wala nyumbani kwake, Tegeta jijini Dar, kwa zaidi ya siku 60 sasa, ambapo kila shabiki wake amekuwa akisema lake, huku Jeshi la Polisi jijini Dar, likitoa tamko kuwa, halina taarifa za kupotea kwake.


BIFU NA MASTAA


Ishu hiyo imeibua mambo mengi, ikiwemo hofu kuwa huwenda Dudu Baya ameuawa kutokana na kuwa na bifu na mastaa kibao Bongo.


Binti wa Dudu Baya aitwaye Maria Godfrey, ndiye aliyefumbua macho ya wengi baada ya kuibuka kwenye mitandao ya kijamii akilalamika kwamba, baba yake huyo haonekani yapata miezi miwili sasa, hivyo kuomba msaada kwenye vyombo vya habari asaidiwe ili apatikane.


Baadhi ya mashabiki wa Dudu Baya, wamekuwa wakihusisha kupotea kwake na bifu zake na mastaa au watu wa kada mbalimbali.


BIFU NA CLOUDS


Wamesema kuwa, kwa nyakati tofauti, Dudu Baya amekuwa kwenye bifu na Clouds Media Group, kuanzia aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds, marehemu Ruge Mutahaba na mtangazaji, Hamis Mandi ‘B Dozen’ ambaye kwa sasa yupo EFM.


Bifu la Dudu Baya na Clouds, lilitajwa kusababishwa na ‘midia’ hiyo kutopiga nyimbo kutoka kwa baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva, hivyo Dudu Baya akavijika cheo cha kuwatetea wenzake.


BIFU NA MADAM RITA


Kutoka hapo, pia inaelezwa kwamba, Dudu Baya aliwahi kuwa na bifu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark Productions, inayoandaa Shindano la Bongo Stars Search, Rita Paulsen ‘Madam Rita’ akimtuhumu kwa utapeli wa pesa za washindi wa shindano hilo la kuzalisha vipaji vipya nchini.


Katika bifu hilo, Dudu Baya alitumia mitandao ya kijamii, kumchafua Madam Rita kwa kadiri alivyoweza.


BIFU NA MR NICE


Bifu lingine la kukumbukwa la Dudu Baya, ni lile lililomhusisha yeye na msanii mwenzake, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’ ambapo aliwahi kumtandika makonde stejini kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar.


MSURURU WA BIFU NA WENZAKE


Msururu wa wasanii wenzake wanaotajwa kuwa kwenye bifu naye, ni pamoja na Khaleed Mohammed ‘TID’, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, Nurdin Bilal ‘Shetta’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’ kisa tu jamaa huyo alijitoa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ambayo Dudu Baya aliapa kulinda ‘brandi’ yake kwa kumshambulia kila atakayekuwa kinyume na matakwa yao.


Wengine wanaotajwa kuwa kwenye bifu na Dudu Baya, ni Barakah The Prince, Chege Chigunda, Madee, Rostam (Roma na Stamina), Nandy, Gigy Money, Young Killer, Baba Levo, Idris Sultan, Steve Nyerere na wengine kibao.


POLISI WANASEMAJE?


Juzi, gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu ambaye aliomba apewe muda wa kufuatilia.


Alipotafutwa kwa mara nyingine Kamanda Taibu alisema amefuatilia, lakini watendaji wake wamesema hawana taarifa zozote za Dudu Baya.


“Nimefuatilia taarifa za huyo msanii kukamatwa hapa kituoni kwangu, lakini hakuna taarifa zozote,” alisema Kamanda Taibu.


KAMANDA MAMBOSASA


Gazeti hili halikuishia hapo, kwani lilimtafuta pia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa ambaye naye alisema kuwa hana taarifa zilizoripotiwa juu ya kupotea kwa mtu huyo.


HADI JANA…


Hadi jana, Dudu Baya alikuwa hajulikani mahali alipo tangu alipopotea Agosti 13, mwaka huu.