Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli ameahidi endapo atapatiwa ridhaa na watanzania ya kuongeza kwa miaka mitano ijayo ataongeza mishahara kwa watumishi wa umma.

 

Dkt. Magufuli amesema hayo leo, Oktoba 25 akiwa katika kampeni zake Mkoani Manyara ambapo amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza amefanikiwa kuongeza vituo vya afya nchini na kupunguza gharama za watu kukimbilia kutibiwa nje ya nchi.


"Nimejitolea kuwatumikia, kama sadaka yangu kwa Watanzania. Ili nikienda mbinguni nikaseme nilijitolea kwa watu hawa. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutaboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na kupandisha mishahara", amesema Dkt. Magufuli .


Ameongeza kuwa, “Tunu yetu tuilinde, Oktoba 28 ukachague viongozi wanaohubiri amani na umoja wa nchi kwa maendeleo ya taifa na tusichague watu wasiojua thamani ya muungano wetu”.