Na John Walter-Babati
Waziri mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye amesema katika vyama vya siasa vilivyopo kwa sasa Tanzania, hakuna chama chochote ambacho kinaweza kutenda mambo yanayofanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Sumaye amesema yeye alipoenda upinzani alifikiri ni gari lenye magurudumu ili walivute liweze kukimbia, lakini badala yake akakuta kuwa ni pancha tupu.
Ameyasema hayo Mjini Babati wakati akimnadi mgombea Ubunge wa Chama cha Mapinduzi mjini Babati Paulina Gekul katika kampeni iliyofanyika katika uwanja wa Papaa.
"Kipindi cha Kampeni kuna mambo mengi ambayo yanaonekana na yasiyoonekana, na kuna watu wengine kipindi cha kampeni wanavunja ndoa zao na baada ya kampeni ndipo wanapogundua kuwa maneno hayo yalikuwa ya uchonganishi" alisema Sumaye
Amewataka wakazi wa Manyara wapuuze maneno ya watu wanaomsema vibaya mgombea Ubunge Paulina Gekul na Mgombea Urais John Magufuli kwa kuwa viongozi hao ndo waliowasogeza mbele kwa kasi kubwa katika maendeleo ya Mji wa Babati.
Amewaambia watu wa Jimbo la Babati kuwa wamepata lulu baada ya kamati kuu kuwarudishia mgombea ambaye anaijua Upinzani na anaijua Ccm, hivyo wasiichezee Lulu hiyo.
"Paulina ni Lulu, msije mkafanya mchezo kwa ajili ya maneno ya wapitao"
Aidha Sumaye amesema hakuna Muujuza wowote unaoweza kutokea Magufuli kushindwa katika Uchaguzi mkuu wa Mwezi Oktoba 28 mwaka huu.
Amewihimiza wakazi wa Babati kuhakikisha wanampigia kura John Pombe Magufuli pamoja na wabunge na madiwani wa Ccm ili waweze kumsaidia katika kusukuma Maendeleo ya nchi.