Na Ahmad Mmow, Lindi. 

Ununuzi wa mazao ya kilimo nje ya mfumo rasmi ambao katika mikoa ya Lindi na Mtwara unajulikana kwa jina la kangomba umetajwa kuwa ni hatari kwa maisha ya wakulima na uchumi wa nchi.

Hayo yameleezwa leo na mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi( CCM) wa mkoa wa Lindi, Abass Matulilo katika kijiji cha Hotelitatu, kata ya Mandawa, wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika wilaya ya Kilwa.

Matulilo ambaye ni maarufu kwa jina la Chigogolo alisema wagombea  na viongozi wanaowahaidi wananchi kwamba wakichaguliwa wataruhusu ununuzi wa mazao kwa njia ya kangomba hawawatikii mema wakulima. Kwani mfumo huo licha ya kuwa ni unyonyaji lakini pia unahatarisha usalama wa wakulima.

Alibanisha kwamba baadhi ya wakulima wakorosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara wanauwezo wa kuzalisha tani 70 za zao hilo. Kwahiyo wakiuza kwa njia ya ulanguzi wanaibiwa fedha nyingi. Lakini pia usalama wao unakuwa hatarini kwasababu wanalipwa fedha taslimu mikononi badala ya benki.

Alisema wakulima wanaouza mazao kwa mfumo huo ni rahisi kuvamiwa na majambazi ambao licha ya kuwapora wanaweza kuwauwa. Kwahiyo viongozi wa vyama na wagombea  wanaohubiri kuruhusu mfumo huo hawawatakii mema wakulima.

" Hata hivyo baadhi ya wanaoahidi hivyo nakusema mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani haufai walikuwa ndani ya serikali hii, lakini mbona hawakushauri hadi walipohama au kufukuzwa!  kama niwakweli na wanahuruma na wakulima wangeshauri na kueleza faida ya kangomba," alisema Matulilo.

Mjumbe huyo wa halmashauri kuu ya taifa(MNEC) ya CCM alitaja sababu nyingine ya mfumo huo kuwa hatari ni kwabaadhi ya wanunuzi kununua mazao kwakutumia fedha bandia. Kitendo ambacho ni hatari kwa uchumi wa wakulima na nchi.

Aidha Matulilo alitoa wito kwa wanachama wa CCM wilayani humo waondokane na tabia ya kuendeleza makundi yanayotokana na mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama hicho. Kwamadai kwamba yanasababisha kipoteze ushindi katika nafasi za udiwani na ubunge katika wilaya hiyo.

Alisema wanaosababisha CCM kipoteze ubunge katika majimbo ya Kilwa Kusini na Kasikazini na udiwani katika kata mbalimbali siyo nguvu za upinzani bali wanachama wa chama hicho. Kwani idadi ya wanachama wa vyama vya upinzani wilayani humo ni ndogo kuliko idadi ya wana CCM.

Kwamasikitiko makubwa Matulilo alisema ni jambo lisilo kubalika kuona chama hicho kinapoteza viti vya udiwani na ubunge wakati serikali imetatua changamoto nyingi. Ikiwemo kwenye sekta za elimu, afya na miundombinu. Vitu ambavyo vinaonekana kwa macho. Kwahiyo CCM wilayani humo kinajinyonga chenyewe.

Kwa upande wake mgombea wa ubunge wa jimbo la Kilwa Kusini, Ali Kasinge alisema akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo atasimamia suala la mikopo kwa vijana, walemavu na wanawake na elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya wajasiriamali.

Lakini pia mgombea huyo alisema atasimamia na kupambana ili wananchi hasa vijana waweze kujiajiri kupitia maliasili zilizopo wilayani humo. Ikiwemo sekta za madini, misitu na uvuvi kwa kujenga viwanda vitakavyotumika kuchakata mazao yanayotokana na maliasili hizo. Kwakufanya hivyo wananchi watapata ajira za moja kwa moja au njia mbadala kutokana na viwanda hivyo.

Kasinge aligusia migogoro ya ardhi kwakusema atahakikisha wananchi wanapimiwa maeneo yao na kupewa hati miliki. Hivyo anaamini migogoro itapungua kwakiasi kikubwa kama siyo kumalizika kabisa. Huku akiweka wazi kwamba yote hayo yanawezekana. Bali kilichosababisha yasiwezekane ni kukosekana dhamira na nia ya dhati ya kushughulikia kero za wananchi wa jimbo hilo.

Alikwenda mbali kwakusema katika nafasi ya ubunge kwa takribani miaka kumi hapakuwa na Mbunge makini anayetokana na chama makini ambacho kingeweza kushughulikia changamoto mbalimbali katika jimbo hilo. Lakini yeye ni mtu makini anayetokana na chama makini. Kwahiyo apewe nafasi hiyo ili atuatue kero na changamoto kwa kutumia ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 ambayo imeeleza na  kuhaidi kuboresha na kushughulikia changamoto zilizopo katika kila sekta.