Serikali na wadau mbalimbali wameipogeza Benki ya NMB kwa msaada wake mkubwa wakulisaidia Taifa na wateja wake kukabiliana na changamoto za janga la COVID-19 ambalo athari zake kiuchumi na kibiashara zinaendelea kuitikisa dunia.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha wakati wa hafla ya Mtandao wa Wateja
Wakubwa wa Benki hiyo ‘NMB Executve Network’ uliyowaleta pamoja wateja zaidi ya 100 wa Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa mitatu ikiwemo Tanga na Kilimanjaro.
NMB ilitangaza unafuu wa ulipaji mikopo kwa wateja wake mwezi Mei mwaka huu, kupitia likizo ya marejesho ya mikopo yao na wengine wakiongezewa muda wa kulipa mikopo hiyo ili kuwasaidia kukabiliana na madhara yaliyoletwa na COVID–19 katika biashara zao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Longido – Frank Mwaisumbe alisema NMB iliwasaidia sana wateja wake na imeendelea kuwa nao karibu wakati wote wa kipindi cha COVID-19 na wao kama Serikali wanawapongeza kwa hilo. Ni jambo kubwa hasa kwa Sekta ya Utalii ambayo imeathiriwa sana na COVID-19. Siyo hivyo tu, Frank vilevile aliipongeza Benki hiyo kwa utaratibu wake wa kukutana na wateja jambo ambalo alisema linasaidia kuboresha mahusinao kati ya Benki na wateja wao.
Naye Afisa Mkuu wa Huduma Jumuishi wa NMB – Nenyuata Mejooli alisema, Benki ya NMB ilitoa ahuweni kwa wateja wake ili kuhakikisha shughuli zao zinastahimili misukosuko ya COVID-19 ikiwemo kubadilisha mfumo wa urudishaji mikopo kulingana na ukubwa wa athari.
Wakati huohuo, Nenyuata, aliwapongeza wateja wao kwa ukakamavu waliouonyesha kipindi cha COVID-19 na kuahidi kuendelea kuwa nao bega kwa bega. “Tunaelewa katika kipindi hiki,biashara kama utalii na sekta ya hoteli zilipata changamoto. Sisi kama NMB tumehakikisha tupo karibu zaidi nanyi wateja wetu ili kuhimili changamoto hizo zilizojitokeza,” aliongeza.
Wiki hiyohiyo, NMB pia iliweza kuwakutanisha wateja wadogo na wa kati walioujiunga na mtandao maalumu wa ‘NMB Business Club’ na kuwapa elimu ya masuala ya kibenki ikiwemo mifumo mipya ya malipo kupitia NMB Mkononi, Mastarcard QR pamoja na huduma zingine za Benki kama Bima (NMB Bancassuarance).
Tangu kuanzishwa kwa NMB Business Club miaka sita iliyopita, mtandao huo upo kwenye Mikoa ya; Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Mtwara, Mbeya na Dodoma huku washirika wake wakiwa zaidi ya 600.
The post Benki ya NMB yapongezwa kwa kutoa ahueni wakati wa COVID-19 appeared first on Bongo5.com.