MEFAHAMIKA kuwa Yanga ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa klabu ya Interclube ya nchini Angola, Carlos St’enio Fernandez maarufu kwa jina la Carlihnos.

Yanga kama ikifanikisha usajili wa straika huyo itakuwa imefi kisha wachezaji kumi wapya katika kuelekea msimu ujao wengine ni Yacouba Sogne, Yassin Mustapha, Zawadi Mauya, Kibwana Shomari.

Wengine ni Bakari Mwamnyeto, Waziri Junior na Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Tuisila Kisinda na Tonombe Mukoko waliosajiliwa juzi usiku huko DR Congo.


Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano,Yanga ipo katika hali nzuri za kukamilisha usajili wa kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya aina tatu.

Video zake zinaonyesha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, ana uwezo wa kufunga mabao kwa njia ya kichwa, kumchambua kipa na kupiga mashuti ya umbali wa kilomita 20.

Ilionekana pia kuwa upo uwezekano mkubwa wa nyota huyo kutua nchini na wachezaji wenzake wa AS Vita, Tonombe na Tuisila ambao usajili wao umefanikishwa na Injinia, Hersi Said.

“Carlihnos ni kati ya wachezaji waliokuwa kwenye mazungumzo na Yanga watakaokuja kuiimarisha safu nzuri ya ushambuliaji baada ya Yacouba na Tuisila usajili wao kukamilika.

“Hivyo mazungumzo yanakwenda vizuri kati ya wakala wa mchezaji na uongozi wa Yanga kupitia kwa Hersi ambaye hivi karibuni alikutana na mchezaji mwenyewe na kupiga picha naye,” alisema mtoa taarifa huyo.

Hersi hivi karibuni aliliambia gazeti hili kuwa: “Tumepanga kusajili wachezaji saba wa kigeni ambao tayari tunaendelea kuufanyia kazi na kikubwa tunachotaka ni kusajili wachezaji vijana wenye ubora watakaoitumikia Yanga kwa muda mrefu.