Waziri wa viwanda na biashara Innocent Bashungwa ameipongeza Benki ya NMB kwa utoaji wa elimu ya kifedha bure kwa wajasiriamali mbalimbali kwenye maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Waziri wa Viwanda na Biashara – Innocent Bashungwa(aliyevaa fulana nyekundu) akisikiliza mafunzo ya elimu ya kifedha yaliyokuwa yakitolewa kwenye banda la NMB, katika viwanja vya Nyakabindi mkoa wa Simiyu kwenye maonesho ya nane nane.Kulia kwa Bashungwa ni Waziri wa Kilimo – Japhet Hasunga na Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi – Sospeter Magesse(aliyevaa koti).

Bashungwa alisema kuwa jambo ambalo linalofanywa na benki hiyo kwenye maonesho hayo ni muhimu sana hasa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji ambao wana uhitaji mkubwa wa elimu ya usimamizi wa fedha.

Waziri huyo alisema hayo jana baada ya kutembelea banda la Benki hiyo wakati wa maonesho hayo, ambapo alifurahishwa kukuta wakulima, wafugaji na wavuvi wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo.

Alisema kuwa lengo kubwa la serikali kuanzisha maonesho hayo ni kutaka wananchi walioko kwenye sekta ya kilimo kuweza kupata teknolojia za kuwawezesha kuongeza tija kwenye uzalishaji wao pamoja na mikopo.

“ Wamekuwa wakipata hizi teknolojia lakini bado tatizo lipo kwenye kujua wapi wapate mikopo, lakini pia jinsi ya kusimamia pesa zao, nimefurahishwa sana kuona hili NMB mnalitekeleza kwa ufanisi hapa Nanenane,” alisema Bashungwa.

Hata hivyo Waziri huyo aliiomba benki hiyo kutoa elimu kama hiyo kwenye vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) ambavyo vimekuwa na matatizo ya ubadhilifu wa fedha za wanachama.

Waziri wa Viwanda na Biashara -Innocent Bashungwa, akizungumza kwenye banda la NMB, katika viwanja vya Nyakabindi mkoa wa Simiyu kwenye maonesho ya nane nane. Wakimsikiliza ni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (katikati) na Meneja wa NMB kanda ya Magharibi Sospeter Magesse.

“ Niwaombe NMB kuweza kuisadia serikali kutoa elimu hii kwa Amcos, baadhi yake bado zina matatizo kwenye usimamizi wa fedha, ingawa serikali tumeendelea kupambana nalo lakini elimu hii ni muhimu sana kwao,” alisema Bashungwa.

Kwa upande wake Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse, alisema kuwa benki hiyo imeweza kutoa kiasi cha sh. Bilioni 161 kwenye mazao ya Tumbaku, Kahawa na Pamba tangu mwanzoni mwa mwaka katika kanda hiyo.

Magesse alisema kuwa kiasi hicho cha pesa kimepelekwa kwenye mazao hayo kama mkopo ambapo wanufaika wakuu ni wakulima kupitia vyama vyao vya msingi (Amcos) takribani 700.

#MWISHO.

The post Waziri Bashungwa aipongeza NMB utoaji elimu ya kifedha Nanenane appeared first on Bongo5.com.