Na John Walter-Simanjiro
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Simanjiro Mkoani  Manyara, wakishirikiana na Jeshi la Polisi mkoani humo,  wamefanikiwa  kuwakamata madereva watatu wa malori kwa tuhuma za kula njama na watumishi wa Halmshauri hiyo kukwepa kulipa ushuru wa mazao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa Takukuru mkoani hapa Holle Makungu, magari hayo  yenye usajili T 450 AZP, KCM 411 L na KCU 073X yalikamatwa yakiwa na shehena kubwa ya magunia ya vitunguu huku stakabadhi za EFD zikionyesha kuwa wamelipa serikalini ushuru kidogo ukilinganisha na magunia ya vitunguu yaliyokuwa yamebebwa.

Makungu amesema awali walipokea tuhuma juu ya watumishi hao Joachim Soka na Peter Sanga  kuwa wanahusika  kuhujumu uchumi wa Halmashauri kwa kutoa risiti  za POS inayovonyesha idadi ambayo ni nusu ya magunia ya vitunguu yanayokuwa yanasafirishwa kwa malori, ambapo huchukua  ushuru wa magunia yanayozidi na  kuingiza fedha hizo mifukoni mwao.

Amesema Takukuru kwa kushirikiana na jeshi la polisi waliweka mtego uliofanikisha kubaini hilo  Kutokana na  Malalamiko waliyoyapokea na kwamba uchunguzi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vya Sheria kujibu tuhuma hizo za kula njama na kuisababishia hasara Halmashauri.

Makungu amesema kuwa Madereva wa malori hayo na Mtumishi Joachim Soka aliyekuwa zamu agosti 12 mwaka huu wanashikiliwa wilayani  humo.

Hata hivyo ameeleza kuwa  watumishi wengine 11 wamefunguliwa Mashtaka katika Mahakama mbalimbali mkoani Manyara kwa kuhusika na vitendo vya rushwa.

Makungu amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa manyara kuwa sehemu ya kupinga vitendo vya rushwa ili kuitokomeza.