Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yakiwamo mashtaka saba ya kuongoza genge la uhalifu, kupanga mikakati ya ugaidi na kutumia sare za jeshi isivyo halali.

Washtakiwa hao, Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya, walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Shedrack Kimaro, Mawakili wa Serikali Waandamizi Wankyo Simon na Tulimanywa Majigo.

Wankyo alidai kuwa katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wote kati ya Mei Mosi na Agosti Mosi, mwaka huu, katika hoteli ya Aishi, Moshi mkoani Kilimanjaro na katika maeneo mengine ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, kwa pamoja na wengine ambao hawakuwapo mahakamani, kwa makusudi walitengeneza mpango wa kutengeneza mikakati ya kigaidi ambayo ni kufanya milipuko katika vituo vya mafuta na mikutano ya hadhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya Tanzania.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa tarehe na maeneo tajwa, washtakiwa hao kwa pamoja na wengine ambao hawakuwapo mahakamani, walishiriki vikao vya mikakati huku wakijua vina muunganiko wa matukio ya ugaidi.

Matukio waliyodaiwa kupanga ni kufanya milipuko katika vituo mbalimbali vya mafuta na mikutano ya madhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakili aliendelea kudai kuwa shtaka la tatu linamkabili Kasekwa ambaye anadaiwa Agosti 5, mwaka huu, katika eneo la Rau Madukani, Moshi, alikutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 3.18, shtaka ambalo pia linamkabili mshtakiwa Lingwenya anayedaiwa kukutwa na Heroin zenye uzito wa gramu 1.06.

Katika shtaka la tano, Kasekwa anadaiwa Agosti 5 katika eneo la Rau Madukani, alikutwa na bastola yenye namba A 5340 aina ya Luger bila ya kuwa na kibali cha umiliki na katika shtaka la sita, Kasekwa anadaiwa kukutwa na vilipuzi ambavyo ni risasi tatu bila ya kuwa na leseni ya umiliki

Katika shtaka la saba, Hassan anadaiwa Agosti 10, katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi, alitumia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Ilidaiwa kuwa sare hizo zilikuwa suruali ya JKT, suruali nne, fulana moja, koti la mvua, jaketi, kofia tano, maovaroli matano, begi la kubebea vifaa lijulikanalo kwa jina la ponjoo, vyeo vinne vya koplo, mikanda minne, soksi pea moja, sweta, beji ya mafunzo ya parachuti, kibuyu cha kunywea maji vyote vikiwa ni mali ya JWTZ pamoja na kisu aina ya AK 47 CCCP.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Kimaro alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo itatajwa Septemba 2, mwaka huu, na washtakiwa walipelekwa mahabusu.