Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemteua Rais John Magufuli kuwa Mgombea Urais wa Tanzania na Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. 


Wagombea hao wa CCM wameteuliwa leo Jumanne tarehe 25 Agosti 2020 baada ya kurudisha fomu za uteuzi za NEC sambamba na kukidhi masharti ya kikatiba.

  

Akitangaza uteuzi huo, Jaji Semistocle Kaijage, Mwenyekiti wa NEC amesema, tume hiyo imewateua baada ya kujiridhisha wamekidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


“Fomu za uteuzi zimejazwa kwa ukamilifu na kwa idadi inayotakiwa na ziada, wagombea wametoa tamko la kuwa wanazo sifa za kugombea, katibu mkuu wa chama ametoa tamko la uthibitisho wa kuwateua wagombea, wagombea wamedhaminiwa na wapiga kura katika mikoa 10 iliyokuwa inatakiwa na mingine mitano ya ziada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


“Wasimamizi wa uchaguzi wamethibitisha majina ya wagombea, wagombea wametoa tamko mbele ya jaji kuwa wanazo sifa za kugombea, wamewasilisha stakabadhi ya dhamana ya Tsh milioni 1, wamewasilisha nakala picha nne za passport size, wametoa tamko la kutekeleza na kuheshimu maadili ya uchaguzi. 


“Baada ya kujiridhisha kwa mujibu wa sheria ya taifa ya uchaguzi na kwa mamlaka niliyopewa na Katiba ya nchi na kanuni za uchaguzi wa mwaka huu,  ninatamka kuwa tume imewateua Dk. John Pombe Magufuli na Samia Suluhu Hassan kuwa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Kaijage.