Na Amiri Kilagalila,Njombe
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Njombe,imefanikiwa kuwahoji baadhi ya watia nia wa Ubunge wa majimbo,Viti maalum na Udiwani waliokuwa wakigombea nafasi katika mchakato uliokamilika hivi karibuni huku wakihusishwa na vitendo vya rushwa.

Katika taarifa ya kipindi cha mwezi Aprili-Juni 2020, iliyotolewa na mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Njombe Bi,Domina Mukama kwa waandishi wa habari,amesema wamefanikiwa kuwafuatilia watia nia wote wakiwa kwenye harakati za kutafuta ridhaa huku baadhi yao wakihojiwa na kuchukuliwa maelezo yaliyopelekwa katika ngazi nyingine kwa ajili ya maelekezo zaidi.

“Tumeweza kuwafuatilia watia nia wote wa Ubunge wa majimbo,viti maalum na udiwani  wakiwa kwenye harakati zao za kutafuta ridhaa kutoka kwa wajumbe watakao wapigia kura,baadhi yao wamehojiwa na hatua stahiki zilichukuliwa dhidi yao”alisema Domina Mukama

Vile vile amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wameendelea na zoezi la urejeshaji wa fedha zilizokuwa zimefanyiwa ubadhiliwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika,SACCOS,AMCOS na NJOCOBA.

“kwa kipindi cha mwezi April –Juni 2020 tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Shs.1,001,060,703.99.Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wananchi wote wa mkoa wa Njombe waliojitokeza kulipa madni na ninaendelea kuwaomba wale wote ambao hawajatimiza kulipa madeni yao waendelee kulipa na kuyamaliza kabisa ili wawe huru.Na kwa wale waliotoroka au kukimbia waelewe tu kwamba serikali ina mkono mrefu na tutawakamata popote pale walipo”aliongeza Mukama

Aidha TAKUKURU mkoa wa Njombe imesema kwa kipindi cha mwezi April hadi Juni wamefanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu,afya na maji.

“Katika ya elimu tulikagua ujenzi wa madarasa 4 na ofisi 4 shule ya sekondari Matola halmashauri ya mji wa Njombe,madarasa 3 shule ya sekondari Mabatini halmashauri ya mji Njombe,Ujenzi wa madarasa 3 shule ya sekondari Igima halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe,Ujenzi wa bweni la wasichana shule ya sekondari Maguvani halmashauri ya mji Makambako,ujenzi wa wa madarasa shule ya sekondari Makonde katika halmashauri ya wlaya ya Ludewa na ujenzi wa jengo la udhibiti elimu halmashauri ya wilaya ya Makete”alisema Mukama

Katika sekta ya afya amesema miongoni mwa majengo waliyokagua ni pamoja na ujenzi wa zahanati ya Kitole katika halmashauri ya wilaya ya Njombe,Ujenzi wa zahanati Isindagosi Wanging’ombe.

Amesema katika sekta ya maji walifanya ukaguzi wa mradi wa maji Matamba-Kinyika katika halmashauri ya wilaya ya Makete,huku miradi yote iliyokaguliwa imetekelezwa vizuri.

Hata hivyo ametoa rai kwa wananchi katika kipindi hiki hiki cha uchaguzi kutokubali kurubuniwa kwa namna yoyote kwa kupewa rushwa ya fedha au kitu chochote kinacholenga kutoa ushawishi wa kupigiwa kura na wagombea.