KUPATIKANA KWA MTOTO ALIYEIBWA.
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JUMA KALINE [32] Mkazi wa Mapele Malangamilo Wilaya ya Chunya kwa tuhuma za wizi wa mtoto SEVERINE GODFREY [03] Mkazi wa Mwaoga.

Ni kwamba mnamo tarehe 08.08.2020 majira ya saa 20:20 usiku huko Kitongoji cha Mwaoga, Kata ya Makongolosi, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mtoto SEVERINE GODFREY [03] Mkazi wa Mwaoga aliibwa wakati akicheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao na JUMA KALINE [32] Mkazi wa Mapele Malangamilo na kumpeleka kusikojulikana.

Baada ya taarifa kufika Polisi, tulifanya msako maalum kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo mbalimbali na mnamo tarehe 09.08.2020 majira ya saa 10:30 asubuhi mtuhumiwa alikamatwa akiwa amembeba mtoto huyo huko maeneo ya Kasument, Kata ya Makongolosi, Wilaya ya Chunya. Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kumuiba mtoto huyo.

Chanzo cha tukio kinachunguzwa. Mtoto amefanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika Zahanati ya Makongolosi na kukutwa akiwa salama kiafya. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.

KUPATIKANA NA BHANGI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lupa BRIAN JOSEPH @ LUHINDA [17] kidato cha tano na mkazi wa Lupa kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi gramu 25.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 09.08.2020 majira ya saa 19:30 usiku huko maeneo ya Shule ya Sekondari ya Lupa iliyopo Kijiji cha Ifuma, Kata ya Lupa, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya akiwa anaripoti shuleni hapo kuanza masomo ya kidato cha tano ambapo alitiliwa mashaka na katika upekuzi alikutwa na kete 05 za bhangi zenye uzito wa gramu 25. 

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KOSA LA KUJERUHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia NYAMA MASELE NGULA [55] Mpagani na Mkazi wa vikae katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za kujeruhi watu wawili kwa kuwakata na vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao ambao ni 1. SAMSON SEMBA [21] Mkazi wa Luhanga na 2. NCHIMIKA PETER [34] Mkazi wa vikae.

Ni kwamba mnamo tarehe 08.08.2020 majira ya saa 09:00 asubuhi huko Kijiji cha Vikae,  Kata ya Igava, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, mtuhumiwa akiwa ameongozana na wenzake jamii ya wafugaji walifika eneo ambalo kulikuwa na ngoma za asili maarufu kama “CHAGULAGA” na walianza kulazimisha waondoke na binti aitwaye KULWA D/O LUHANGA [14] Mpagani na Mkazi wa Vikae ili aende kuishi na MAYOMBI NYAMA kama mke wake.

Kutokana na hali hiyo, majeruhi/wahanga walikuwa wakiwazuia watu hao kuondoka na binti yao aitwaye KULWA LUHANGA [14] ambapo washukiwa hao walikwenda kukusanya watu wengine jamii ya kifugaji zaidi ya 20 kwa ajili ya kumchukua binti huyo kwa lengo la kumuoza kwa mtu aitwaye MAYOMBI NYAMA lakini ndugu/wazazi wa mtoto huyo waliendelea kupinga kitendo hicho na ndipo walishambuliwa sehemu mbaimbali za miili yao na watuhumiwa.

Kiini cha tukio hilo ni kutorosha binti aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake bila hidhini ya wazazi. Watuhumiwa walikutwa na vielelezo ambavyo ni Powertiller moja ambalo lilitumika kubeba mtuhumiwa na watuhumiwa wengine, mlanga mmoja, na marungu mawili yaliyotumika kujeruhi wahanga wa tukio hili.

Msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine unaendelea, Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI - SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA