Mamlaka ya Somalia inasema watu 10 wamefariki wakati wa majibishano ya risasi nje ya gereza la Mogadishu.

Msemaji wa wizara ya habari alisema mahabusu sita ambao walikuwa wanamgambo wa kundi la kigaidila Al-Shabab waliuliwa na askari wanne pia waliuawa.

Chanzo cha majibishano ya risasi ni jaribio la mahabusu mmoja kutaka kutoroka.

Kuna taarifa zinazosema mahabusu mmoja aliweza kupora bunduki kutoka kwa msimamizi wa gereza na baadae mahabusu na wafungwa wengine walivunja chumba cha kuhifadhia bunduki.

Kikosi maalum cha polisi kilipelekwa kukabiliana na ghasia hizo ambazo zilikua zinalenga kuvunja gereza.

Gereza hilo lina wafungwa ambao ni wanamgambo maarufu wa al-Shabab ambao wanatumikia kifungo cha maisha au kunyongwa.

Tukio la namna hiyo lilifanyika mwaka 2017.

The post SOMALIA: Watu 10 wauawa katika jaribio la mahabusu wakivunja gereza na kutaka kutoroka appeared first on Bongo5.com.