Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeitaka Radio Free Africa (RFA) kutoa maelezo ya utetezi kimaandishi na kufika mbele ya kamati kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka Kanuni za Huduma za Utangazaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Maudhui ya TCRA, Julai 29 mwaka huu redio hiyo inatuhumiwa kuwa ilikiuka kanuni hizo kupitia kipindi cha “Amka na BBC” kwa kurusha maudhui bila kuzingatia mizania ya habari.

Katika kipindi hicho walimhoji Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu juu ya viongozi wa chama hicho kutoshiriki katika kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa.

Imeelezwa redio hiyo ilirusha taarifa ya Lissu akitoa tuhuma na kulalamika kuwa serikali ilimnyima nafasi ya kutoa heshima za mwisho bila kumtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali ili aweze kutoa ufafanuzi, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Kutokana na kitendo hicho, RFA wanatuhumiwa kukiuka Kanuni Na. 15(2) (b) na (c) na 16 za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni) 2018.