Mkuu wa zamani wa Kanisa Katoliki, Papa Benedict XVI, anaripotiwa kuumwa sana baada ya kumtembelea kaka yake aliyekuwa mgonjwa nchini Ujerumani mwezi Juni na sasa hali yake ni dhaifu sana.

   
Gazeti la Passauer Neue Presse la nchini Ujerumani limeripoti kwamba Papa Benedict mwenye umri wa miaka 93 anasumbuliwa na ugonjwa unaotokana na kirusi kinachosababisha pelepele usoni na maumivu makali, kwa mujibu wa mwandishi wa tawasifu ya Papa huyo, Peter Seewald.

"Kwa mujibu wa Seewald, Papa kwa sasa ana hali dhaifu sana," limeandika gazeti hilo. "Akili na uwezo wake wa kufikiri bado viko makini lakini sauti yake inasikika kwa shida sana."

Seewald alimtembelea Papa Benedict mjini Rome siku ya Jumamosi (Agosti 1) kumkabidhi tawasifu yake.

"Kwenye mkutano huo licha ya kuumwa kwake, Papa alikuwa na matumaini na akasema kwamba endapo hali yake itaimarika, atachukuwa kalamu tena aandike," limeandika gazeti hilo.

Papa Benedict alimtembelea kaka yake mgonjwa aitwaye Georg nchini Ujerumani mwezi Juni, ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya Italia tangu alipojiuzulu ghafla upapa mwaka 2013.

Georg Ratzinger alifariki dunia wiki mbili tu baada ya hapo, akiwa na umri wa miaka 96.

Papa huyo wa zamani, ambaye jina lake halisi ni Joseph Ratzinger, sasa anaishi kwenye nyumba ndogo ya watawa mjini Vatican.

Tangu awe papa wa kwanza kujiuzulu kwa takribani miaka 600 iliyopita, amekuwa haonekani sana hadharani kutokana na hali yake ya kiafya.

Akiwa mwanamapokeo wa Kanisa Katoliki, nafasi yake ilichukuliwa na mwanamageuzi Papa Francis.