Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa CHADEMA Tumaini Makene amesema kuwa tukio la ofisi za chama hicho Kanda ya Kaskazini kuchomwa moto na wasiojulikana si jambo jema ukizingatia leo Mgombea Urais wa chama hicho Tundu Lissu atakuwa Arusha.


Makene ametoa kauli hiyo hii leo Agosti 14, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kuongeza kuwa na hata mlinzi wa ofisi hizo mpaka sasa hivi hajulikani alipo na hata simu zake hazipatikani.


"Taarifa za awali usiku wa kuamkia leo watu wasiojulikana wamevamia na kumwagia Petroli jengo la Ofisi za Kanda ya Kaskazini,  na bahati mbaya hata mlinzi wa ofisi hizo hajulikani yuko wapi baada ya tukio hilo, ni tukio baya kwa sababu hata mgombea wetu wa Urais anaingia Jiji la Arusha leo" amesema Makene.


Ofisi za chama hicho Kanda ya Kaskazini zimeungua moto usiku wa kuamkia leo, baada ya watu wasiojulikana kumwagia Petroli jengo hilo na kisha kulilipua.