Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia Rafael Grossi anatarajia kwenda Iran wiki ijayo kwa mara ya kwanza tangu aanze kuliongoza shirika hilo mwezi Desemba mwaka uliopita. 


Mkurugenzi huyo wa shirika la IAEA anakwenda Iran katika muktadha wa kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa dhidi ya nchi hiyo juu ya mpango wake wa nyuklia. 


Lengo la ziara ya Rafael Grossi ni kuweza kupata kibali cha kuyatembelea maeneo ya nyuklia yanayodhaniwa kuwepo tokea mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla Iran haijatia saini mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 baina yake na mataifa makubwa ya dunia. 


Shirika la IAEA limesema Iran inatuhumiwa kuwa imehifadhi au imetumia nyenzo za kinyuklia kwenye sehumu hizo bila ya kutoa taarifa. 


Mkurugenzi wa shirika hilo amesema katika tamko kwamba lengo hasa ni kulitatua suala la kuweza kuyatembelea maeneo hayo. 


Iran imesema inatumai ziara hiyo itaongeza ushirikiano baina yake na shirika hilo la kimataifa. Wiki iliyopita Marekani iliimarisha shinikizo kwa kuupa taarifa Umoja wa Mataifa kutaka vikwazo vyote dhidi ya Iran viendelezwe.