Aliyekuwa mama wa taifa wa Marekani Michelle Obama amesema kuwa ana tatizo la sonona kwasababu ya janga la virusi vya corona, ubaguzi wa rangi na unafiki wa utawala wa Trump.

Alisema kukabilia “hisia zinazobadilika-badilika” kunahitaji “kujielewa binafsi” na “yale yanayokuletea furaha”.

Bi. Obama alisema anapitia matatizo na amekuwa na changamoto ya kuendeleza ratiba yake ya kufanya mazoezi ya viungo na kulala.

 

“Ninaamka usiku wa manane kwasababu nina wasiwasi juu ya kitu fulani au nawaza kuhusu mzigo mzito ninaoubeba moyoni.”

Alisema maneno hayo wakati wa kipindi chake cha pili alipokuwa anamuhoji mwanahabari wa Marekani Michele Norris.

“Huu sio wakati mzuri, kiroho,” Bi. Obama alisema. “Najua ninakabiliana na kiwango fulani cha sonona.

“Sio tu kwasababu ya karantini, lakini kwasababu ya ubaguzi wa rangi, na kushuhudia tu utawala huu, na kutazama unafiki ndani yake, kila uchao, kunavunja moyo.”

Pia alisema kwamba “inachosha” “kuamkia tena taarifa za mwanaume mweusi au mtu mweusi ambaye kwa namna fulani anafanyiwa matendo ya kinyama, au mtu anamdhuru, au ana uawa, au anashutumiwa kwa madai ya uwongo.”

“Na hilo limenisababishia mzigo ambao sijawahi kuuhisi maishani mwangu, kwa muda,” amesema.

Hata hivyo alisema, “kuwa na ratiba ni jambo la msingi” kukabiliana na hisia hizi – na kwamba kudumisha ratiba hiyo kumekuwa hata muhimu zaidi wakati huu wa janga.

Kipindi chake cha kwanza alimuhoji mume wake Barack Obama, ambaye alikuwa madarakani kabla ya Donald Trump.

The post Michelle Obama: Nina tatizo la sonona (depression) sababu ya corona, ubaguzi wa rangi na unafiki wa utawala wa Trump appeared first on Bongo5.com.