Maambukizi ya wastani ya virusi vya corona yaliyoripotiwa Afrika wiki iliyopita yamepungua kulingana na Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa (CDC Afrika).

Wastani wa maambukizi yalioyiropitwa wiki iliyopita yalikuwa 10,300 ikilinganishwa na wiki iliyotangulia ambapo idadi ilikuwa 11,000.

Mkurugenzi wa kituo cha CDC Afrika, Dkt. John Nkengasong amesema hiyo ni “ishara ya matumaini”.

Afrika imerekodi maambukizi 1,147,369 zaidi ya nusu ya maambukizi hayo yanatoka Afrika Kusini, na vifo takriban 26,000.

Dkt. Nkengasong alisema ana matumaini “maambukizi yameanza kupungua” lakini akaongeza kwamba ni mapema mno- tunakabiliana na kirusi kibaya zaidi kinachosambaa kwa haraka mno”.

“Taarifa hizi tunazipokea kwa tahadhari,” alisema, akielezea kwamba hakutaka watu waanze kuona ugonjwa wa virusi vya corona umetoweka na kuacha kuchukua hatua za kuuzuia usisambae.

“Hatutaki kizazi chetu kione kwamba tunapunguza kasi ya hatua za kukabiliana na ugonjwa huu.”

Alitaka watu kuendeleza juhudi zao za kuzuia maambukizi ya virusi na hususan kusema kwamba watu wanahitajika kuendelea kuvaa barakoa, kutokaribiana na pia idadi ya wanaopimwa inastahili kuongezeka.

Je Afrika inastahili kusherehekea?

Anne Soy, BBC News, Nairobi

Baada ya idadi ya wanaothibitishwa kupata maambukizi kuongezeka barani Afrika, wiki hizi ambazo zimeshuhudia kupungua kwa idadi ni faraja kubwa.

Lakini hilo linastahili kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.

Hivi karibuni, idadi ya wanaopimwa imekuwa ikiongezeka hadi zaidi ya milioni 10, kulingana na kituo cha CDC Afrika.

Hiyo ni karibu asilimia 1 ya idadi ya watu barani Afrika.

Hata hivyo, Afrika Kusini inaongoza kwa idadi ya wanaopimwa na wanaothibitishwa kupata maambukizi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibisha kuwa idadi ya maambukizi mapya imekuwa ikipungua nchini Afrika Kusini siku za hivi karibuni.

Lakini pia kupungua kwa idadi ya wanaopimwa, kuna maanisha kwamba vigumu kupata picha kamili ya jinsi ilivyo.

Huenda ikawa ni mapema mno kutabiri kuwa idadi ya wanaothibitishwa kupata maambukizi mapya itaendelea kupungua.

Dkt. Nkengasong pia alisema kwamba zaidi ya vipimo milioni moja vimekuwa vikifanyika kote barani humo huku Afrika Kusini ikiwa moja ya inayopima watu kwa wingi zaidi.

Idadi ya maambukizi na vifo imepungua ikilinganishwa na sehemu zingine duniani kama vile Ulaya, Amerika Kusini na Marekani ambayo pekee imerekodi visa zaidi ya 5,500,000, lakini baadhi ya wataalamu wameonya kwamba huenda kukawa na maambukizi zaidi ya vilivyorekodiwa Afrika kwasababu ya ukosefu wa vipimo.

Usambaaji wa virusi unaonekana kupungua Afrika lakini tangu mwanzo wa janga idadi ya maambukizi ilikuwa chini kisha ikaanza kuongezeka taratibu hasa Afrika Kusini.

Afrika Kusini imerekodi maambukizi 596,060 ya virusi vya corona, kulingana na data ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins. Hii ni zaidi ya nusu ya maambukizi Afrika na ni nchi ya tano katika orodha ya zile zenye idadi kubwa zaidi ya maambukizi duniani.

Hata hivyo idadi ya maambukizi nchini humo imekuwa ikipungua. Kilele cha ugonjwa huo, zaidi maambukizi 12,000 mapya yalikuwa yakirekodiwa kila siku, na idadi hiyo imepungua hadi wastani wa maambukizi 5,000.

Nchi ya Afrika nyengine itakayoingia kwenye orodha hiyo ni Misri, ambayo ni ya 31 katika orodha ya dunia kwa maambukizi 96,914.

The post Matumaini yaanza kujitokeza bara la Afrika, baada ya kuelezwa maambukizi ya Corona kupungua appeared first on Bongo5.com.