UKIHADITHIWA tu na mtu yeyote unaweza kusema ni hadithi ya kutungwa, lakini ukweli ni kwamba kuna watu huko kwenye visiwa vya Papua New Guinea ambavyo vimezungukwa na bahari inayoitwa Bismarck Sea wanakula binadamu wenzao.

Nchi hiyo yenye watu wapatao milioni 7.3 ina makabila mengi yanayotofautiana mila. Tena basi mengine yana mila mbaya na za kutisha na wanakiuka haki za binadamu kwa kiasi kikubwa. Katika mapori wanaoishi watu hao ni jambo la kawaida mtu ‘akionwa’ na wazee wa kimila kwamba ni mchawi, huteswa kwa kuchomwa na silaha zenye ncha kali lakini baya zaidi humalizwa kwa kukatwakatwa kisha kufukiwa kwenye shimo.

Yapo makabila mengi katika visiwa hivyo ambavyo vipo mashariki ya mbali, karibu na Indonesia na Australia. Baadhi ya makabila yanaishi maisha duni na ya enzi ya ujima. Kuna kabila ambalo mwanamke akifiwa na mume, hukatwa kidole kimoja, akifiwa na mtoto, hukatwa kidole kingine, huwa hivyo hata ukifiwa watoto watano, basi vidole vitano vitakatwa.


Wenyewe wanasema hiyo ni njia ya kuomboleza eti kwamba uwe na uchungu halisia baada ya kufiwa na ndugu yako wa damu, mtoto au mume. Haijaelezwa kwa nini wanaokatwa vidole huwa ni wanawake tu maana hata picha kwenye mitandao, wengi wa waliopoteza vidole wanaoonekana ni wanawake, tena wale wazee au wakongwe!

Makabila yanayofanya vitendo hivyo yameelezwa kuwa ni ya Dani na Kuru ambayo mengine yanapatikana katika nchi ya Indonesia pia. Inaelezwa inapotokea mtu amefariki dunia, mama mhusika huitwa na kuingizwa katika chumba maalum na kuulizwa anataka akatwe kidole gani.


Akionesha, kidole hukatwa bila sindano ya ganzi kwa pigo moja ya panga yenye makali na kupakwa dawa za mitishamba kisha mama aliyekatwa hutoka ndani huku akilia na ndipo waombolezaji wengine hudakia kulia kwa nguvu.Baada ya kidole kukatwa ncha iliyokatwa pamoja na kucha, huchomwa moto na wazee wa kimila huku wakiimba nyimbo za makabila yao.

Mara baada ya zoezi hilo kinachofuata na kidole kuchomwa moto na kuwa jivu kisha majivu yake huwekwa kwenye chombo maalum na baadaye hufuata zoezi la majivu hayo kupakwa nyuso za waombolezaji wote ambao wapo kwenye msiba huo.

Kwa kawaida watu hao hawavai nguo na badala yake hutumia magome ya miti na wanaume hufunika dhakari yao kwa aina fulani ya vibuyu. Kuna vibuyu vina ‘mkono’, basi hutumia mikono hiyo kuingiza kwenye dhakari na kuifunga kwa njia ya kitamaduni, lakini sehemu nyingine za eneo hilo nyetu huachwa wazi na hupita hata mbele ya watoto wao bila kuona haya!

Kwa upande wa wanawake, wao hufunika nyeti zao kwa magombe ya miti na matiti yao huachwa wazi vila kufunika chochote!

Kabila la Kuru wao kama aliyefariki dunia alikuwa ni kiongozi, basi ubongo wake hutolewa na kuliwa na wanaume.