Jeshi la Mexico limemkamata kigogo mwenye mtandao mkubwa wa madawa ya kulevya nchini humo, Jose Antonio Yepez, aliyesaidia kuchochea vurugu zilizoipa majaribu makubwa Serikali ya Rais, Andres Manuel Lopez Obrador.

Kigogo huyo aliyefahamika kwa jina la utani kama El Marro au The Mallet, alikamatwa Jumapili iliyopita, kwa mujibu wa vyanzo vya Serikali.

Imeelezwa kuwa Yepez aliongoza genge kubwa la dawa za kulevya linalojiita ‘Santa Rosa de Lima’ ambalo limetengeneza ngome ya vijana wanaochochea vurugu nchini humo.

Vyombo vya usalama vimeongeza kuwa alifanikiwa kuliunganisha kundi lake na kundi linalotuhumiwa kufanya matukio ya mauaji linalojiita CJNG, ambalo ni moja kati ya makundi ya kihalifu yenye nguvu kubwa nchini humo.

Tukio hilo la kukamatwa kwa Yepez, ni moja kati ya mafanikio kwa Rais Obrador, ambaye aliahidi kubomoa ngome za makundi ya kihalifu nchini humo, lakini badala yake alipoingia madarakani Desemba 2018 matukio ya kihalifu yalionekana kuongezeka.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo imeeleza kuwa Yepez alikamatwa akiwa na watu wengine watano.

Imeeleza kuwa ilifanikiwa kumuokoa mwanamke mmoja mfanyabiashara aliyekuwa ametekwa na kundi hilo, pamoja na silaha nzito za kundi hilo la kihalifu.