Ikiwa imesalia wiki moja kabla ya kampeni za uchaguzi kuanza nchini Tanzania, wawania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatarajiwa kujua hatma yao hii leo. Chama hicho tawala kiko katika matayarisho ya kuwapata wagombea wake katika ngazi zote baada ya kupitisha wagombea wa urais mwezi uliopita.

Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa nchi, Dkt. John Pombe Magufuli hapo jana aliongoza Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, Dodoma, kwa lengo la kuandaa agenda ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa hii leo.

Kikao hicho na cha leo ni mwendelezo wa safari ya CCM kupata wagombea wa nafasi mbali mbali kuelekea uchaguzi wa hapo Oktoba 28.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitakuja na matokeo yasiyotarajiwa kwa baadhi. Yapo majina ambayo yalipita yakiwa ya kwanza kwa kura za wajumbe lakini yatakatwa, badala yake yatapitishwa majina mengine.

Pia, zitashuhudiwa sura mpya kuiwakilisha CCM katika majimbo, huku baadhi ya sura kongwe zikidondoshwa.

Tafsiri ya hilo ni kwamba zile kura za wajumbe sio maamuzi ya mwisho kwa CCM, bali kura hizo hutoa mwongozo wa awali katika kufanikisha mchakato mzima hadi kulipata jina moja la mgombea atakayepambana na wagombea wa vyama vya upinzani.

Kwanini majina hukatwa?

Moja kati ya sababu ya majina kukatwa, hata yale yaliyopata ushindi wa kwanza katika kura za wajumbe ni ushawishi wa mgombea. Vyama vya kisiasa daima hutafuta urahisi wa kushinda. Mgombea ambaye huonekana ni mzigo kwa chama hata kama wajumbe walimpitisha kwa kura nyingi, uwezekano wa kupitishwa katika vikao vinavyofuata unakuwa mgumu sana.

Wanachama wa CCM

Maadili ya mgombea ni jambo jingine linalozingatiwa. Ni karata muhimu kwa wanaosaka nafasi ya kuiwakilisha CCM. Maadili yanaweza kumuinua aliyepata ushindi wa tatu ama wa pili na kumzamisha aliyepata wa kwanza.

Katika mchakato wa uchaguzi wa awali, mambo yalikuwa ya uwazi sana. Kura zilihesabiwa bila kificho, kila mchukua fomu akavuna alichopanda. Licha ya uwazi katika mchakato huo, bado malalamiko kuhusu vitendo vya rushwa yalizuka.Rushwa inaweza kuwa sababu nyingine ya jina la mgombea kukatwa. Wale wanaoshinda kura za wajumbe kwa kutumia mbinu hiyo, ikibainika ni rahisi majina yao kutupwa na kuangaliwa majina mengine yaliyo safi.

Ina maana kuwa, hadi CCM inamkabidhi mgombea wake wa mwisho kuipeperusha bendera ya chama, mchakato na mchujo wa majina unakuwa mrefu sana. Na hiyo ndio siasa ya uchaguzi ndani ya CCM.

Athari ni zipi?

Waswahili husema vita vya panzi ni sherehe kwa kunguru.

Mchakato unaoendelea sasa huenda ukaangusha baadhi ya vigogo wa CCM.

Yamkini vipo vyama vya upinzani vinavyotarajia kuvuna makada au wafuasi kutoka chama tawala. Hali hiyo imetokea katika chaguzi zilizopita na baadhi ya waliokatwa CCM wakakimbilia upinzani na kushinda, ingawa wapo pia ambao walishindwa hata baada ya kwenda upinzani.

Wakati uchaguzi wa awali ulipofanyika, kulisambaa baadhi ya video zikiwaonesha wafuasi wa CCM wakiwakataa baadhi ya wagombea ambao ni vigogo.

Swali, itakuwaje ikiwa maamuzi ya mwisho yataleta majina ya wale ambao wanakataliwa na wapiga kura wa chama hicho?

Mchakato wa sasa ni mtihani mkubwa kwa chama tawala; kati ya mapenzi ya wapiga kura, chaguo la wajumbe na maamuzi ya mwisho ya kikao cha halmashauri kuu.

Athari ni, ikiwa wafuasi watapelekewa mgombea ambaye hana mvuto tena, anakataliwa hadharani. Kifuatacho ni chama kupoteza kura nyingi huku nyingine zikienda kwa upinzani. “Ama tegemea wapiga kura ambao watakwenda katika visanduku na kuchagua kwa shingo upande.

Mbali ya hilo, mgombea atakaye pitishwa wakati alipigwa vita, atakuwa na kazi kubwa na ya ziada ya kuirudisha imani ya hao wapiga kura wake. Lakini kazi kubwa zaidi itakuwa ni kuwashinda wagombea wa vyama vya upinzani.

Wafuasi wa CCM Tanzania

CCM na Upinzani

Hali ya hewa ya uchaguzi huu inaashiria kuwa CCM imedhamiria kushinda kwa kishindo ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Kuanzia katika nafasi ya urais hadi wagombea wa majimboni. Lengo ni kupata viti vingi kuliko walivyo navyo sasa.

Dhamira hiyo inasukumwa na kile wanachoamini wana CCM kwamba Rais Magufuli kaifanyia makubwa Tanzania, kuanzia ujenzi wa miundombinu, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na hili la karibuni nikitaja kwa uchache, ni kuipeleka nchi katika uchumi wa kati dhaifu.

Hivyo hesabu za CCM ni kuhakikisha Rais Magufuli anashinda muhula mwingine, ili akaendelee na ujenzi wa nchi. Na kupatikana kwa wingi wa Wabunge kutasaidia katika kupitisha mambo mbali mbali huko Bungeni.

Lakini hadithi ni tofauti kwa upande wa upinzani; Rais Magufuli anaangaliwa kwa jicho tofauti kabisa. Wanaamini ni mgombea ambaye hapaswi kuendelea kuiongoza nchi. Kuna msururu wa mambo ambayo kwa upinzani haya kwenda sawa, kuanzia kupigwa marufuku maandamano, mikutano ya hadhara ya kisiasa, kamata kamata ya viongozi, pamoja na kukithiri kesi mahakamani dhidi yao katika kipindi cha miaka mitano.

Kwa sura hiyo kila upande unajiandaa na uchaguzi huu kwa joto la aina yake.

CCM haitaki kukosea katika mchakato wa kuwapata wagombea. Pia vyama vya upinzani vinajitayarisha kwa imani ya kumng’oa madarakani Rais Magufuli na sera zake ambazo zinalalamikiwa kuminya demokrasia.

The post Fahamu mchakato wa kuwapitisha wagombea kwenye kikao cha kamati kuu appeared first on Bongo5.com.