Dan Matakaya alikuwa kwenye usingizi mzito pale ghafla alipohisi uchungu mkali kama wa kuchomwa na moto usoni.

Tahadhari: Baadhi ya picha huenda zikakuogofya

Alizinduka ghafla kwani mwanzoni alidhani ilikuwa tu ndoto ya kuogofya. Lakini mwasho ulioandamana na uchungu ulizidi kumwandama. Aligundua kwamba ilikuwa si njozi, ni mambo yaliyokuwa yakitendeka katika uhalisia.

Kwa kutatizika, aligundua chanzo cha uchungu ule kilikuwa tindikali, na mhusika alikuwa mkewe.

Matakaya alikuwa ni afisa wa polisi aliyekuwa anahudumu katika kituo kimoja kaunti ya Kisii nchini Kenya wakati kisa hicho kilipotokea alfajiri mnamo 21 Septemba, 2013.

“Aliponimwagilia tindikali, nilijaribu kila niwezalo kufikia maji angalau yanitulize. Lakini mke wangu aliyamwaga kwenye sakafu. Palikuwepo na nyaya zilizokuwa wazi ambazo ziligusa yale maji,” anaeleza

“Ni kana kwamba alikuwa na nia ya kuhakikisha kuwa nimepigwa na umeme. Nilipiga mayowe hadi majirani wangu walipoitikia kilio changu. Ni wao walionikimbiza hospitalini.”

Kwa bahati mbaya ile tindikali ilikuwa imemeng’enya ngozi yake kwenye sehemu ya uso na kichwani, kwa kiasi kikubwa.

Dan Matakaya
Kuna kipindi Dan Matakaya alitaka kujitoa uhai

Matibabu na upasuaji

Alipofikishwa hospitalini Kisii, alipewa huduma ya kwanza na baadaye akawa anatibiwa ila madaktari hawangeweza kumtibu zaidi.

“Nilipewa huduma ya kwanza, uso wangu ulioshwa na wakati huo nilikuwa na uwezo wa kuona, japo uchungu ulikuwa mwingi mno kwenye mwili wangu. Wahudumu walijaribu kunipa tembe za kupunguza maumivu,” Dan anakumbuka.

Baada ya siku mbili alihamishwa hadi hospitali ya Kakamega alipokaa kwa siku mbili na baadaye kuhamishwa hadi hospitali ya taifa ya Kenyatta.

Dan anasema kuwa akiwa hospitali ya kwanza baada ya muda alipofuka kabisa.

“Inavyoonekana ni kuwa ile tindikali iliendelea kunidhuru macho yangu hata baada ya kemikali ile kuoshwa na kupanguswa usoni mwangu,” amesema.

Katika hospitali ya Kenyatta, alilazwa kuanzia Septemba 2013 hadi Februari 2014 ambapo alifanyiwa upasuaji mara kadha. Anakadiria kwamba alifanyiwa upasuaji mara 15.

Dan anasema kuwa madaktari walikuwa wanatoa nyama na ngozi kutoka sehemu nyengine za mwili wake na kuzipandikiza sehemu ambazo alikuwa ameathirika mno.

Upasuaji aliyofanyiwa ulikuwa unamtuliza lakini hali ya kupona iliendelea kwa mwendo wa polepole mno.

Dan Matakaya pia alipewa nesi ambaye alimuhudumia kwa miezi 6 wakati alipopewa ruhusa kurejea nyumbani.

Kazi ya nesi ilikuwa kuosha vidonda alivyokuwa anauguza.

Haikuchukua muda kabla yake kuzidiwa na kurejeshwa katika hospitali ya Nairobi West kwani vidonda vilianza tena kuuma na havikuwa vinakauka. Akiwa mle hospitalini alifanyiwa upasuaji mwengine.

“Japo majeraha yanayotokana na kuchomwa na tindikali yalikuwa yanapona, kulikuwa bado na matatizo ya viungo vyangu. Kwa mfano mikono yangu ilikuwa imepona, lakini ilikuwa migumu mno kukunjana, shingo pia ilikuwa imepona ila ilikuwa ngumu kiasi kuwa singeweza kuigeuza wala kuinamisha kichwa kama ada,” Dan anasema.

Changamoto nyengine ilikuwa ni sehemu ya pua lake, wataalam walifanya upasuaji ili kufungua mashimo yanayotoa na kuingiza hewa lakini yalifungana siku kadhaa kabla ya mwisho wa mwaka wa 2014.

Mwaka wa 2015, alirejea tena hospitali ya Kenyatta, ambapo alifanyiwa upasuaji mwengine kwenye pua lake kwani operesheni ya kwanza haikusaidia kutuliza hali.

Mnamo Septemba 10 mwaka wa 2019 alifanikiwa kupata mdhamini ambaye alikubali kufanikisha upasuaji mwengine.

Mdhamini mwenye ni Faceforwad International ambalo ni shirika linalosaidia waathiriwa wa dhuluma za kinyumbani na wengineo.

 

Mnamo tarehe 4 Septemba 2019 alisafiri hadi Jimbo Califonia Marekani, ambapo alifanyiwa upasuaji wa pua na pia marekebisho ya uso katika hali ya kuunyorosha.

Upasuaji huu, Dan anasema, ulihusu kuopoa mafuta kwenye tumbo lake na kuyadunga kwenye sehemu za uso ilikusaidia ngozi iwe laini.

Dan alirejea nchini Kenya tarehe 1 mwezi wa kumi mwaka wa 2019.

Dan alitazamia kusafiri hadi nchini Marekani ili kufanyiwa upasuaji mwengine wa pili mwaka huu lakini hajaweza kusafiri kutokana na marufuku za usafiri kutokwasababu ya ugonjwa wa Covid-19.

Changamoto za Dan anasema la kwanza ilikuwa kujikubali na muonekano wake wa sura ulivyo kwa wakati huu.

Vilevile kukubali kuanza maisha upya bila kuona kutokana na kupofuka.Dan Matakaya

Dan Matakaya alipofuzu mafunzo ya polisi

Kutaka kujitoa uhai

Dan Matakaya alikuwa amewazia kujitoa uhai wake madaktari walipomweleza kuwa hatakuwa na uwezo wa kuona tena.

Wakati ule alikuwa katika hospitali ya Kenyatta.

“Baada ya jaribio la pili la kufungua pua langu kufeli, madaktari walianza kupoteza matumaini jinsi ya kunisaidia,” anasema.

“Kuna wakati nilihisi tu nijirushe kutoka urofa ya juu ya hospitali kuu ya Kenyatta nife. Wakati huo nilikuwa katika orofa ya tisa hospitali ya Kenyatta,” Dan anasema.

Japo anasema kuwa sauti nyengine ilikuwa inamnong’onezea kuwa, ‘Je, ukijirusha chini na ukose kufa itakuwaje’?

Dan Matakaya
Baada ya kutafakari tena kuhusu kujiua Dan Matakaya aliona Mungu ana mipango mema juu yake

Tumaini baada ya dhiki

Aliona hakukuwa na haja ya kujitoa uhai na akagundua kuwa angali na mchango katika ulimwengu huu.

“Nilianza kufikiria mawazo ya kuishi, huku nikipata nasaha kutoka kwa wataalamu wa afya kiakili. Nilianza kuelewa utamu na uzuri wa maisha kama zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu,” Dan anasema

Mwaka wa 2016 aliunda wakfu wa Dan Shieshie. Huu ni wakfu ambao huwasaidia wanaume wanaojipata katika ndoa au mahusianoambayo wanadhulumiwa.

Pia ni nafasi ya wanaume kueleza uzoefu wao kwenye ndoa na jinsi ya kukabiliana na matatizo kwenye ndoa.

“Mimi ninaelewa kuwa wanaume wanaonekana kana kwamba wao ndio wanaoanza dhuluma na vita vya kinyumbani. Lakini inapogeuka na kuwa kinyume hata jamii yenyewe haijui ifanyeje nini kwani haiko tayari kusikiliza masaibu ya wanaume wanaodhulumiwa,” Dan anasema.

Ingawa bado anahudumu kama polisi, yeye huwa anafanya kazi za ofisini kutokana na makovu usoni na athari za kuchomwa kwa tindikali.

Chanzo BBC.

The post Dan Matakaya: Nilimwagiwa tindikali na mke wangu nikiwa nimelala (Tafadhali picha zilizopo zakuogofya) appeared first on Bongo5.com.