LICHA ya miluzi kupigwa mingi na kubaki kuwa kitendawili kisichokuwa na majibu juu ya binti atakayeolewa na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, baba yake staa huyo, Abdul Juma ‘Baba D’ ameibuka na kutoa baraka zake kwa staa wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’, IJUMAA WIKIENDA linakupa mchapo.Ukaribu wa Zuchu na Mondi, uliibuka siku chache baada ya kusainiwa kama second lady wa lebo hiyo, kiasi cha mashabiki kujiuliza mara kadhaa, nini kinaendelea kati yao, kwani ni tofauti na ilivyokuwa kwa wasanii wengine waliosajiliwa kwenye lebo hiyo.MASWALI KIBAO

Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijiuliza kulikoni, maana sehemu nyingi wamekuwa wakionekana kuwa pamoja hasa kwenye sherehe kadhaa. “Zuchu na Mondi wamekuwa karibu sana au kuna ndoa inanukia? Maana Mondi ameahidi kuoa mwaka huu, tena siku ya bethidei yake, isije ikawa ni Zuchu ndiyo anaolewa,’’ alisema Shabiki mmoja wa staa huyo.KULALA NYUMBA MOJA

Kama hiyo haitoshi, mara kadhaa Mondi na Zuchu wamekuwa wakionekana kwenye chumba ambacho analala staa huyo namba moja Bongo, huku pia ikielezwa kuwa, bibie huyo amekuwa akiangusha usingizi kwenye mjengo huo wa kifahari uliopo Mbezi Beach jijini Dar.BABA D AFUNGUKA

Baada ya mambo kuwa mengi, IJUMAA WIKIENDA lilifanya jitihada za kumtafuta baba mzazi wa staa huyo mkubwa, ambapo yeye bila hiyana, alionesha kubariki ndoa hiyo, huku akieleza kuwa ni jambo la kheri. “Japo hilo suala la Diamond kumuoa Zuchu hajanitaarifu, lakini mwisho wa siku ndoa ni jambo kubwa na zuri maishani, hivyo kama wataoana itakuwa ni kheri.KUHUSU MCHUMBA MWINGINE?

“Kuhusu mchumba wake mwingine, nalo sijui na hata kama yupo ambaye ataolewa na Diamond, ni sawa tu maana yule ni mtoto wa Kiislamu na dini yake inamruhusu kuoa hata wake wanne maana uwezo huo anao,’’ alisema Baba D.WAZAZI WENZA WA MONDI…

Mbali na hilo, Baba D alizungumzia ishu ya Mondi kutokuoa wanawake aliozaa nao watoto wanne, ambapo alisema jambo hilo hawezi kulizungumzia. “Kuhusu Diamond kutokuoa hao wazazi wenziye aliozaa nao, sijui kitu na hata sielewi,’’ aliongeza.

KAULI YA MONDI

Akizungumza kwenye vyomba vya habari hivi karibuni, Mondi alikaririwa akisema kuwa yupo singo kwa sasa, lakini anahitaji kuingia kwenye ndoa. Kabla ya maneno hayo aliyoyasema hivi karibuni, mkali huyo aliwahi pia kunukuliwa kuwa ataoa Oktoba 2, mwaka huu siku ambayo ni bethidei yake.

Hata hivyo, licha ya watu wengi hususan mitandaoni kuamini kuwa atamuoa Zuchu, hivi karibuni kuliibuka mluzi mwingine baada ya binti mmoja wa Rwanda kuibuliwa na kuelezwa kuwa ndiye atakayemuoa.ZARI NAYE AHUSISHWA

Mbali na huyo, upo pia ‘upepo’ uliochezeshwa na mzazi mwenziye Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye naye alihusishwa na jambo hilo la ndoa hususan baada ya wawili hao kuonekana kwenye mawasiliano mazuri siku za hivi karibuni.Mapema wiki iliyopita, Zari alitupia gari jipya aina ya Brabus B63-620 ambalo ameliandika BABA LAO kwenye plate number, huku akisikika akitamka kuwa mkoko huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1, atampa Mondi siku akienda Sauz anapoishi.TUJIKUMBUSHE

Zuchu alisajiliwa rasmi miezi mitano iliyopita akiongeza idadi ya wasanii kwenye lebo hiyo inayojumuisha wasanii wengine kama Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, Abdul Idd ‘Lava lava’, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ na Yusuph Mbwana ‘Mbosso’.

STORI: HAPPYNESS MASUNGA, DAR