YANGA inayonolewa na Kocha Mkuu, Luc Eymael, leo inashuka uwanjani kumenyana na Lipuli kwenye mchezo mwisho wa Ligi Kuu Bara bila kuwa na nyota wake nane jambo ambalo linamliza kocha huyo.

Nyota hao wa kikosi cha kwanza ni pamoja na Lamine Moro ambaye anasumbuliwa na majeraha aliumia kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Mapinduzi Balama,Haruna Niyonzima,Papy Tshishimbi hawa wote ni majeruhi.

Patrick Sibomana, mshambuliaji huyu raia wa Rwanda yupo Dar kwa matatizo ya kifamilia, beki kisiki Kelvin Yondani hajaripoti kambini, Deus Kaseke yeye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliipata kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na Bernard Morrison kiungo ambaye yupo kwenye mgogoro na  Yanga kuhusu mkataba wake.

Eymael amesema kuwa ni wakati mgumu ambao anapitia kwa sasa kwa kuwa anaingia vitani bila kuwa na silaha za kazi zile ambazo anazitegemea.

“Nipo kwenye wakati mgumu kwa sasa, ninamaliza mchezo wa mwisho na malengo yakiwa ni kumaliza tukiwa nafasi ya pili naona mambo magumu, sina Lamine, Kaseke ambaye ana kadi, Tshishimbi, Haruna, Balama hawa wote ni majeruhi.Yondani hata sijui yupo wapi,Morrison najua tabia yake inajulikana, sijui itakuaje?,” alisema.

Lipuli inapambana kusaka nafasi ya kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 44 haina uhakika wa kubaki ikiwa itapoteza huku Yanga ipo nafasi ya tatu inapambania nafasi ya pili ikiwa na pointi 69 sawa na Azam FC iliyo nafasi ya pili wakitofautina mabao ya kufunga na kufungwa zote zimecheza mechi 37.