WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii na Wazee Ummy Mwalimu amefunga kambi ya wagonjwa wa Corona iliyokuwa Lulanzi Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani. 

 Akifunga kambi hiyo jana ambapo alisema,  kati ya kambi 85 zilizokuwa zinahudumia wagonjwa wa Corona zimebaki 11 ambazo nazo zinaendelea kufungwa siku zijazo kutokana na ugonjwa huo kuendelea kutokomea hapa nchini. 

Aliwasihi  wananchi kuacha kujibweteka na kuendelea  kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali ili kuepuka kupata maambukizi mapya. 

“Tumefunga kambi 74 hadi sasa na hii hapa Lulanzi ilikuwa ni Kati ya kambi kubwa ambayo ilikuwa inapokea wagonjwa wengi na leo naifunga rasmi kwani mgonjwa wa mwisho hapa aliruhusiwa Mei 26 hakuna mwingine aliyepokelewa hadi leo” alisema 

Aidha Waziri Ummy aliwataka wakazi wa Kibaha kufika katika Hospitali ya Wilaya kupata huduma na kuondoa hofu ya kuwa kituoni hapo bado kuna wagonjwa wa Corona. 

Alisema, wananchi wanatakiwa kuondoa hofu kwani majengo yote yamefanyiwa usafi baada ya wagonjwa kuondoka katika Hospitali. 

” Lulanzi sio tena kambi ya wagonjwa wa Corona , wananchi ondoeni wasiwasi na mfike kupata huduma za afya, tusikimbilie Tumbi ile ni Hospitali ya Rufaa tungependa ibaki kutoa huduma za hadhi ya Rufaa” alisema Ummy. 

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa Halmashauri ya mji wa Kibaha kusimamia utoaji wa huduma za viwango vinavyostahili kwa wagonjwa. 

Akiongea katika Hospitali hiyo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alimshukuru Rais Pombe Magufuli kwa Hospitali hiyo ambayo imemaliza uhitaji wa Hospitali ya Wilaya aliyokuwa akiiomba kwa zaidi ya miaka saba iliyopita. 

Koka aliwataka wananchi kufika kutibiwa katika Hospitali hiyo ambayo imeondoa kilio cha uwepo wa Hospitali ya Wilaya . 

Alisema changamoto iliyopo katika Hospitali hiyo kwasasa ni pamoja na ubovu wa barabara na gari la wagonjwa ambalo Waziri Ummy aliahidi litapatikana hivi karibuni. 

Mganga mkuu wa Halmashauri ya mji wa Kibaha Tulitweni Mwinuka alisema, Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za kawaida kwa wagonjwa Juni 6 na kwamba jamii bado ina Mashaka kufika katika Hospitali hiyo.