Marekani imeweka rekodi nyingine mpya wa maambukizi mengi ya corona. Kulingana na takwimu za chuo kikuu cha Johns Hopkins, watu 67,000 wamethibitishwa kuambukizwa kwa siku moja.
Marekani ambayo ndiyo nchi inayoongoza ulimwenguni kote kwa idadi ya walioambukizwa virusi hivyo, imekuwa ikirekodi maambukizi ya juu tangu mwisho wa mwezi Juni, haswa kusini na magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa siku 10 zilizopita, idadi ya watu wapya ambao wamekuwa wakiambukizwa nchini humo, wamekuwa kati ya 55,000 hadi 65,000 kila siku.
WHO: Maambukizi ya virusi vya corona yaongezeka ulimwenguni
Wakati huo huo, kuna kile kinachotizamwa kama mvutano kuhusu namna ambavyo serikali ya rais Donald Trump inavyolishughulikia janga hilo.
Mnamo Jumatano, mtaalamu na pia mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza nchini humo Daktari Antony Fauci, alisema haelewi juhudi za baadhi ya maafisa wa Ikulu ya White House kumdharau lakini anaamini hilo ni kosa kubwa.
Mvutano kuhusu corona Marekani

Kwenye mahojiano na jarida la habari la The Atlantic, Daktari Fauci amesema juhudi hizo za maafisa wa White House ni jambo lisilo la kawaida.
Mnamo siku ya Jumanne, Rais Donald Trump alimkosoa mshauri wake mkuu wa masuala ya biashara Peter Navarro, akisema hakupaswa kuchapisha maoni yake makali yaliyomkosoa Antony Fauci, ambaye ni mtaalamu mkuu wa serikali kuhusu masuala ya corona na ambaye pia ni maarufu.
Navarro aliandika kuwa japo Fauci ana uhusiano mzuri na umma, baadhi ya kauli zake ni makosa.
Wakati mwingine, kumeibuka mzozo kati ya Rais Trump na Fauci, huku Trump akitaka kufungua nchi ili watu warudi kazini. Vilevile amekuwa akitaka shule zifunguliwe kwa wanafunzi kuendelea mbele na masomo. Lakini Fauci amekuwa akishauri kuwa hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kuu, ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.
Kwa jumla zaidi ya watu milioni tatu wamethibitishwa kuambukizwa nchini Marekani na zaidi ya watu 137,000 wamefariki tangu janga hilo lilipoanza.
The post Watu 67,000 waambukizwa Covid-19 kwa siku moja Marekani appeared first on Bongo5.com.