Watu wapatao 50 wameuawa kwenye maandamano yanayofanyika katika mkoa wa Oromiya nchini Ethiopia baada ya kuuawa mwanamuziki maarufu nchini humo. Wakati huo huo mwanasiasa wa upinzani Jawar Mohamed amekamatwa.


Watu hao 50 wameuawa wakati walipokuwa wanashiriki kwenye maandamano katika mkoa wa Oromia ambayo yalianza mara baada ya kuuawa mwanamuziki maarufu nchini humo Haacaaluu Hundeessaa. Msemaji wa jimbo hilo Getachew Balcha amefahamisha kwamba watu waliokufa ni waandamanaji na maafisa wa usalama na ameongeza kusema kuwa baadhi ya sehemu za biashara zimechomwa moto.

Wakati huo huo serikali ya Ethiopia imethibitisha kwamba kiongozi maarufu wa upinzani nchini humo Jawar Mohammed amekamatwa. Bwana Mohammed ambaye hapo awali alikuwa mmiliki mkubwa wa vyombo vya habari na aliyejiunga hivi karibuni na chama cha Oromo Federalist Congress alikamatwa hapo jana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa pamoja na watu wengine 34.

Mkuu wa polisi nchini Ethiopia Endeshaw Tassew ameeleza kwamba bwana Jawar Mohammed alikamatwa baada ya kutokea purukushani na polisi kuhusiana na mwili wa mwanamuziki huyo maarufu aliyepigwa risasi siku ya Jumatatu usiku na tukio hilo likasababisha maandamano makubwa nchini humo.

Mkuu huyo wa polisi ameeleza kwamba kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed na wenzake waliingilia kati wakati mwili wa mwanamuziki huyo ulipokuwa unasafirishwa kwa ajili ya mazishi kwenye mji wake wa uzawa wa Ambo. Amesema wapinzani walitaka kuuchukua mwili huo na kuurudisha mjini Addis Ababa ndipo purukushani ilipotokea. Polisi mmoja wa kikosi maalumu kutoka jimbo la Oromo aliuawa.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi watu hao waliokamatwa pia walikuwa na bunduki aina ya Kalashnikov, bastola tano na radio za mawasiliano. Haacaaluu Hundeessaa mwanamuziki kutoka jamii ya Oromo alijulikana kwa nyimbo zake zinazotumiwa sana kwenye maandamano.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed katika ujumbe wake wa Twitter mnamo siku ya Jumanne alitoa rambirambi zake na kuahidi kwamba uchunguzi wa kina utafanyika na wakati huo huo ameutaka umma utulie. Kwingineko kamati ya kuwalinda wanahabari CPJ imelaani kufungwa kwa mtandao wa intaneti mjini Addis Ababa pamoja na kuvamiwa vyombo vya habari vya Oromia.