NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
KAMATI ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Iringa imewata watiania na wanachama kuheshimu kanuni na sheria za uchaguzi zilizowekwa ndani ya chama ili kuepuka panga linaloweza kujitokeza pindi watakapo kiuka taratibu za chama.

Mwenyekiti wa kamati ya siasa Mkoa wa Iringa Abel Nyamahanga ameyasema hayo wakati akizungumza na wandishi wa habari katika ukumbi wa ccm mkoa wa Iringa na kusema kuwa watia nia wanatakiwa kupita ofisi za wasimamizi wa uchaguzi ili kupewa taratibu za uchaguzi.

Nyamahanga alisema chama hakitasita kumchukulia hatua mwanachama na mtia nia ambaye atakiuka sheria na taratibu za uchaguzi.

Alisema kuwa kila kitu kinachofanywa na chama cha mapinduzi kipo kwenye kanuni za uchaguzi za chama hicho hivyo watia nia kwenye ngazi za udiwani na ubunge wanatakiwa kufuata kanuni hizo ili waweze kutia nia bila kuwa na kashfa.

“Tunacho kizungumza hapa kila kitu kipo kwenye miongozo na kanuni za chama chetu cha mapinduzi (CCM) ndio maana tunawataka watia nia wote kufuta kanuni na taratibu za chama wakati wa nia yake ya kutafuta nafasi ya kuwatumiakia wananchi” alisema Nyamahanga

Nyamahanga aliwataka wanachama na watia nia wote kuheshimu kanuni za uchaguzi ndani ya chama cha mapinduzi ili kuondokana na tatizo la rushwa ambalo miaka mingi kipindi cha uchaguzi ndio huaribu taswiara ya chama cha mapinduzi.

Aidha Nyamahanga aliwataka watia nia waache mara moja kupita kwenye kata na matawi kwa lengo la kukutana au kuwasalimia wapiga kura badala yake wanatakiwa kupita katika ofis za wasimamizi wa uchaguzi ili wapate taratibu na mwenendo wa uchaguzi unaokubarika ndani wa chama hicho.

 Alisema wapo baadhi ya watia nia wamekuwa wakiwakusanya  wapiga kura kutoa maeneo mbalimbali kwa kisingio cha kuwasalimia,kujitambulisha  na kuwapa nauli ikithibitika kwa mgombea yoyote yule ataondolewa kwenye orodha ya wagombea kwa mujibu wa ibara ya 35 kifungu kidogo cha kumi na sita.

Kwa upande wake mjumbe wa halmashauri kuu (CCM) Taifa Salim Asas alisema kuwa serikali ya chama cha mapinduzi imeleta maendeleo kwa wananchi hivyo wanauhakika wa ushindi katika uchaguzi mkuu.

Alisema kuwa chama cha mapinduzi mkoa wa Iringa kitashinda kwa kishindo majimbo yote hata jimbo la Iringa mjini ambalo lipo upinzani nalo watashinda kwa kuwa chama hicho kimejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna makundi ili kuhakikisha kwenye uchaguzi mkuu wanaenda kwenye uchaguzi wakiwa wamoja.

Aliongeza kuwa wananchi wa manispaa ya Iringa wamekuwa na imani na utendaji wa kazi wa chama cha mapinduzi hivyo itakuwa kazi nyepesi kushinda kwa kuwa wanauhakika wa kumpata mgombea mwenye uwezo wa kupeperusha pendera ya chama hicho.