Na.Faustine Gimu Galafoni,Kahama Shinyanga.
Sakata la  bati  1346  za msaada  zilizotolewa katika maafa ya mvua ya barafu mwakata  mwaka 2015 limezua mjadala baada ya  fedha zaidi ya Tsh. milioni 12 zilizotokana na  kuuzwa kwa bati hizo   kukosa mwelekeo huku Diwani Mstaafu wa Kata ya Mwakata Ibrahim Six Masanja akihusishwa na ubadhilifu huo.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Julai ,9,2020 katika kijiji cha Mwakata  halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ,baadhi ya wananchi  wa kijiji hicho akiwemo Mathias Mtonja  ,Richard Maganga wamehoji kupatikana muafaka wa fedha hizo zilizotokana na kuuzwa kwa bati za msaada kwani kuna zaidi ya Milioni 12 hazijulikani zilipo  huku akaunti ya kijiji  cha Mwakata ikiwa na salio la Tsh.Laki moja tu hadi sasa.

Wakijibu hoja hizo za Wananchi  ,Mwenyekiti  mteule wa kijiji  cha Mwakata  Mseka Mathias   amesema hajui matumizi ya fedha zilizotokana na kuuzwa kwa bati na kuahidi kulipeleka  ngazi za juu huku mtendaji wa kijiji hicho Mfikwa Andrew  pia naye akishindwa kujibu hoja hizo za bati.

Wananchi hawakuridhishwa na majibu ya afisa Mtendaji wa kijiji cha Mwakata Mfika Andrew kwani wamedai kuwa yeye alikuwa mjumbe wa  ODC na atakuwa  anajua  fedha za bati zilikoenda ,hali iliyosababisha mvutano   katika mkutano huo.

Akihitimisha mkutano huo Mwenyekiti wa kijiji cha Mwakata ,Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga  Mseka Mathias   amependekeza kuunda tume ya watu  wawili na kuendelea  ili kwenda kwa mkuu wa Wilaya ya Kahama Ana Mringi Masha  kuomba kuitisha mkutano utakaohusisha Diwani Mstaafu Ibrahim Six Masanja pamoja na viongozi wengine  wastaafu  ili kuweza kujibu tuhuma hizo   mbele ya Wananchi.

Hata hivyo  Mtandao huu umezungumza na Diwani  Mstaafu wa kata ya Mwakata Ibrahim Six Masanja  ambapo amesema kuwa  bati hizo ziliuzwa kwa kutangaziwa wananchi na waliandika barua  Kwa Mkurugenzi mtendaji ili kupata idhini ya kuuza bati hizo.