SALVATORY NTANDU
Serikali Wilayani Kahama mkoani Shinyanga imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa  Baadhi ya Wakandarasi watakaobainika kufanyakazi kwa Uzembe na kutozingatia Mikataba ya kazi sambamba na wanaojenga  madaraja  na barabara zilizochini ya kiwango ili kudhiti hujuma zinazofanywa na kampuni za ujenzi zinazotanguliza maslahi  mbele maslahi yao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya kahama Anamringi Macha wakati akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo katika zoezi la ukaguzi wa ujenzi wa  barabara na madaraja unaotekelezwa na kampuni ya Hemed Holdings Limited ambayo imepewa kandarasi ya kujenga katika halmashauri ya msalala .

Alisema kuwa Licha ya serikali kutoa fedha kwa wakandarasi wazawa lakini baadhi yao wamebainika kufanya kazi chini ya kiwango ili wapate faida kubwa na kusababisha baadhi ya miradi kuharibika muda mfupi baada ya kukabidhiwa kwa serikali jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

“Kamati ya Ulinzi na Usalama ipo kazini kuhakikisha tunakagua miradi yote ya barabara ili kujiridhisha na ujenzi wake,na hatutasita kumwajibisha mkandarasi asiyezingatia michoro na ramani zilizoainshwa kisheria,kwa mfano katika eneo la nyangalata kunamkandarasi alijenga daraja katika eneo ambalo sio njia ya maji na mvua ziliponyesha maji hayakupita katika eneo hilo na kuisababishia hasara serikali,”alisema Macha.

Alifafanua kuwa endapo barabara za Kagonjwa –Mwankima na Mwakata –Butondoro zikifunguliwa zitasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri kutokana na wakazi wa maeneo hayo kuzalisha mpunga kwa wingi lakini wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la Usafirishaji wa mazao kutokana na baadhi ya barabara kutopitika.

Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijni (TARURA) katika halmashauri ya Msalala Mhandisi Wilfred Muta alisema kuwa mwaka huu mvua zimenyesha kwa wingi na kusababisha wakandarasi wengi kushindwa kamilisha miradi ya ujenzi wa barabara kwa wakati ambapo kuwa kampuni Hemedi Holdings Ltd ilipaswa kukamilisha ujenzi barabara na madaraja hayo kabla ya agosti 15 mwaka huu na gharama za ujenzi huo ni zaidi ya shilingi milioni 200

Nae mhandisi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya hemedi holdings Ltd   Emanuel Sospeter alisema kuwa wameshindwa kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo kutokana na mvua zilizonyesha kwa muda mrefu mwaka huu na mpaka sasa wamefikia asilimia 60 na ifikapo Agosti 15 watahakikisha wamekabidhi mradi huo kwa halmashauri ya Msalala.

Mwisho.