SALVATORY NTANDU
Watu 13 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa tuhuma za kuhusika na tukio la Mauaji ya Watu  Wanne katika Kiwanda cha Kuchenjulia Dhahabu cha Dakires kilichopo katika Mgodi mdogo wa  Namba nne Wisolele katika Halmashauri ya Msalala na Kupora Cabon kilogramu 385.34,Bunduki moja aina ya Short Gun yenye risasi mbili .

Akizungumza na Waandishi wa habari Julai 10 mwaka huu Mkuu wa Oparationi Maalum  za Jeshi la Polisi SACP, Mihayo Mshikhela alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata wahalifu waliohusika na tukio hilo pamoja na mali zilizoporwa katika kiwanda hicho cha kuchenjulia dhahabu zizoibiwa June 30 katika kiwanda hicho.

Alisema kuwa Oparationi hiyo ilanza June 30 mwaka huu baada ya mauaji hayo ambapo jeshi hilo limefanikiwa kukamata pikipiki tano zilizohusika kusafirisha Cabon hizo,Panga moja,na bunduki moja yenye risasi mbili pamoja na watu hao 13 ambao wanahusika kupanga na kutekeleza mauaji hayo.

“Jeshi la polisi limefanikiwa kusambaratisha mtandao wa uhalifu ambapo tumewakamata waliotekeleza mauaji, waliopanga mauaji, waliosafirisha mali za wizi baada ya kupora na waliohifadhi mizigo hiyo ya wizi na tunaendelea kuwatafuta wengine ambao waliotoroka,”alisema Msikhela.

Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kufanya misako katika maeneo yote ya migodi midogo ili kudhibiti matukio hayo na kuwataka wamiliki wa viwanda vya kuchenjulia dhahabu kuacha tabia ya kuzungukana na kuibiana mali kwani uchunguzi wa awali unaonesha yapo matukio mengi ya namna hiyo yanatokea lakini hayajawahi kuripotiwa katika vyombo vya usalama.

Msikhela aliwataja watu hao waliouwawa June 30 mwaka huu majira ya saa tano usiku katika kiwanda hicho kuwa ni pamoja, Juma Jingwasanya (31),Lusajo Michael Mwamasangula (31),Raphal Kipenya Mapinduzi (27) na Daniel  William (25)  huku Exavery Mboya (21) akijeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu katika hopitali ya wilaya ya Kahama.

“Tunatoa rai kwa Mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya Cabon kabla ya kwenda kuchenjuliwa kuhakikisha wanajiridhisha kama imetoka katika  eneo salama kwani wahalifu wanatumia ujanja nao kuomba vibali ili kuchenjua dhahabu za wizi,”alisema Msikhela.

Msikhela pia  ameziagiza Kampuni zote za Ulinzi Nchini kuhakikisha Wanaajiri Walinzi waliopitia mafunzo mbalimbali ya kijeshi ili kuweza kupambana na wahalifu katika maeneo yao ya kazi kwani kumekuwepo kwa matukio ya walinzi kuvamiwa na kuporwa silaha.

Mwisho.