Kulikuwa na hamaki na kukata tamaa katika chumba cha mkutano huo baada ya wikendi nzima ya majadiliano huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwashambulia viongozi wa Uholanzi na Austria na kutishia kuondoka kwenye kikao hicho.
Mazungumzo hayo yasiyokuwa na mapumziko yaliyochini ya uenyekiti wa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel yameshindwa kuleta makubaliano kuhusiana na kiwango na masharti katika kugawanya yuro bilioni 750 miongoni mwa nchi za Ulaya ili kusaidia kuunusuru uchumi wa bara hilo uliporomoka kutokana na janga la virusi vya corona.
Lakini Michel amewataka viongozi hao kujaribu kutafuta suluhu kwa mara ya nyingine.
Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte ameituhumu Uholanzi na marafiki zake Sweden, Denmark, Finland na Austria kwa kuziendea kinyume nchi zengine katika Umoja wa Ulaya.
Lakini Kansela wa Austria Sebastian Kurz amesema watashikilia msimamo wao.
“Hili ni suala muhimu sana kwasababu naamini kwamba hatuwezi tu kukubali kiholela holela. Kuna kiwango flani cha uwezekano wa kubadilisha msimamo katika nchi nyingi ila sisi tumekubaliana tutashikilia msimamo wetu ambao uko wazi na hatuko tayari kwenda chini ya kiwango fulani. Hilo bila shaka litalazimu mijadala mingine kufanyika,” alisema Kurz.
The post Viongozi Umoja wa Ulaya wakesha kuunusuru uchumi baada ya Corona appeared first on Bongo5.com.