Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT Wazalendo imesema kuwa itamuandikia barua aliyewahi kuwa waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, ili aweze kujiunga na chama hicho kwa kile wanachoamini kuwa na yeye ni muhanga wa demokrasia.

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 9, 2020, na  Naibu Katibu wa Itikadi Mawasiliano na Uenezi wa ngome hiyo Massabo Julius, hii ni baada ya wao kumuona Membe akiwa amerejesha kadi yake ya uanachama wa CCM mara baada ya kufukuzwa uanachama huo miezi kadhaa iliyopita.

"Tutaandika barua kwa Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Uongozi wa chama Maalim Seif Sharif Hamad, kuonesha msimamo wetu juu ya hamu ,shauku ya Mh Bernad Membe kujiunga na chama chetu na mwisho tutaandika barua rasmi kwa Mh.Bernard Kamilius Membe, kuonesha ombi letu kwake la kumuomba ajiunge na chama chetu cha ACT wazalendo" imeeleza taarifa hiyo.

Aidha vijana hao wamesisitiza kuwa, "Tunasisitiza msimamo wetu wa kumuomba Mh Membe kujiunga na chama chetu kwasababu ni wajibu wetu kama vijana na wanachama, kwani katiba yetu ibara ya 12(4) inatoa majukumu kwa wanachama kushawishi wananchi kujiunga na chama chetu".