Utafiti uliofanyiwa watoto Ulaya walioambukizwa virusi vya corona umebaini kwamba ni nadra sana kutokea kwa vifo miongoni mwa watoto.

Watoto wanne pekee ndio waliokufa kati ya 582 wawili kati yao walikuwa na matatizo ya kiafya tayari.

Dalili zao zilikuwa za wastani na baadhi yao waliothibitishwa kuambukizwa corona hakuwa na dalili zozote kabisa huku mmoja kati ya 10 akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

Madaktari wanasema utafiti huo ni wa kutia moyo lakini mengi yanahitajika kugunduliwa kuhusu tiba stahiki inayoweza kupewa watoto watakaoonesha dalili zao ni kali mno.

Utafiti huo ulibaini nini?
Watafiti hao walifuatilia hali ya watoto kuanzia waliotimiza siku tatu tangu kuzaliwa hadi miaka 18 wanaoishi katika nchi 25 za Ulaya.

Wote walibainika kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 wakati ugonjwa huo unafikia kilele chake kwa mara ya kwanza Aprili.

Robo ya idadi hiyo walikuwa na maradhi mengine tayari.

Vifo vinne vilivyotokea wakati wa utafiti huo, hakuna ambaye alikuwa na umri wa chini ya miaka 10 na wawili kati ya hao waliokufa walikuwa na matatizo mengine ya kiafya.

Zaidi ya nusu ya watoto walioshirikishwa kwenye utafiti walilazwa hospitali na asilimia 8 wakahitajika kupata huduma kutoka chumba cha wagonjwa mahututi.

Je watoto hao walikuwa na dalili gani?
Asilimia 65 ya watoto hao walionesha homa, asilimia 54 walikuwa na maambukizi upande wa juu wa njia ya upumuaji, asilimia 25 walikuwa na ugonjwa wa nimonia na asilimia 22 wakawa na dalili za matatizo ya utumbo

Asilimia 16 ya watoto ambao wengi wao walipimwa kwasababu ya kuwa karibu na watu waliopata maambukizi ya virusi vya corona, hawakuwa na dalili zozote kabisa.

Athari zake ni zipi?
Watafiti wanasema kiwango cha vifo kwa watoto kuna uwezekano mkubwa kikawa chini kuliko kile kilichojitokeza kwenye utafiti huo kwasababu hadi wakati huo, walio na dalili za wastani huenda hawakuwa wamepimwa au kubainika.

Hatahivyo, data zaidi inahitajika kusaidia madaktari kufanya maamuzi ya machaguo ya tiba stahiki kwa watoto ambao wanauguwa kwasababu ya virusi vya corona, akaongezea.

Dkt. Marc Tebruegge kutoka Taasisi ya Afya ya Watoto London, amesema kuwa idadi kubwa ya watoto na vijana wanadalili za wastani za ugonjwa wa Covid-19.

“Hatahivyo, kuna idadi ya watoto wanaopata maambukizi makali na kuhitajika kupewa huduma ya chumba cha wagonjwa mahututi, na hili linastahili kutiliwa maanani wakati wa kupanga na kutilia kipaumbele raslimali za huduma ya afya wakati janga la corona linapoendelea,” amesema.

Watoto ambao wameambukizwa na viusi vyingine vinavyosababisha matatizo ya kupumua licha ya kwamba wamepata ugonjwa wa Covid-19, walikuwa katika hatari ya kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi.

“Hili linaweza kuwa na athari mbaya msimu wa baridi, wakati ambapo homa na mafua huwa vinajitokeza sana,” amesema Dkt. Begoña Santiago-Garcia kutoka chuo kikuu cha hospitali ya Gregorio Marañón, Madrid, Uhispania.

Utafiti huo umechapishwa katika jarida la masuala ya Watoto na Afya ya Vijana la Lancet.

The post Utafiti: Watoto wengi waliopata corona hawakuonesha dalili, ni wanne tu waliofariki kwa ugonjwa huo kati ya 582 appeared first on Bongo5.com.