Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi ameamuru kuwa wabunge na wafanyakzi wote wa chombo hicho watapaswa kuvaa barakoa katika kipindi chote cha janga la virusi vya corona.

USA | Trump | Impeachment (picture-alliance/dpa/AP Images/M. Rourke)

Akizungumza bungeni jana Jumatano, spika Pelosi amesema anatumai wabunge na wafanyakazi wote wataheshimu sharti hilo kama ishara ya kulinda afya na usalama wa kila mmoja ndani ya majengo ya Bunge.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya mbunge wa chama cha Republican Louie Gohmert aliyepinga vikali uvaaji barakoa kutangaza kuwa ameambukizwa virusi vya corona jana Jumatano.

Kulingana na Pelosi, chini ya kanuni hiyo mpya wabunge wataruhusiwa tu kuondoa barakoa wakati wa kuhutubia au kutoa michango mbele ya Bunge.

Hayo yanajiri wakati Marekani imefikisha idadi ya vifo 150,000 vya COVID-19 ambayo ni kubwa kuliko taifa lingine lolote duniani.

Viongozi wa Ulaya wana mitizamo tofauti 

Spanien Coronavirus Menschen mit Masken (picture-alliance/Zumapress/P. Freire)

Barani Ulaya ambako mataifa kadhaa yametangaza vizuizi vya kusafiri kwenda na kutoka Uhispania, viongozi wake wamejikuta katika vita ya maneno juu ya iwapo kuna umakini katika kushughulikia janga la virusi vya corona.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson muda mfupi tangu alipotangaza amri ya wasafiri wote wanaotoka Uhispania kuwekwa karantini, amesema maeneo mengine ya Ulaya yako kwenyde hatari ya kukumbwa na wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona.

Matamshi yake yamezusha ukosoaji kutoka Ufaransa ambako waziri wa Afya Olivier Veran amesema nchi yake haipo katika kitisho cha wimbi la pili la COVID.19 lakini inachukua tahadhari

“Tunao mpango unaolenga kuyakinga makundi yaliyo katika hatari, kutoa taarifa kwa wingi, kukataza baadhi ya safari isipokuwa zile muhimu kwa lengo la kuzuia kushamiri kwa janga hili na baadae kujikuta katika wimbi la pili la maambukizi” amesema waziri Veran.

Uhispania yajipigia upatu kuwa ni salama 

Virus Outbreak Brazil (picture-alliance/AP Photo/A. Penner)

Nchini Uhispania, taifa lililoyumbishwa vibaya na virusi vya corona, serikali imesisitiza kuwa ni sehemu salama ya kuitembelea na kukosoa uamuzi wa Uingereza wa kuwaweka karantini wasafiri wanaotoka nchini humo.

Huko Brazil serikali imetangaza kuruhusu kuanza tena kwa safari za ndege za kimataifa kwa watalii wa kigeni tangu ilipozifuta mnamo mwezi Machi kutokana na janga la virusi vya corona.

Nchi hiyo ya Amerika ya kati iliyoathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona hajifafanua zaidi kuhusu sababu za kufikia uamuzi huo katika wakati inashika nafasi ya pili nyuma ya Marekani kwa idadi ya vifo na maambukizi ya COVID-19.

Hapo jana serikali ilitangaza vifo vingine 1595 vya COVID-19 na idadi hiyo imekuwa ikipanda kwa wiki ya tano mfululizo huku maambukzi yakisambaa kwenye majimbo mengine nchini humo.

The post Spika wa Bunge Marekani aamuru Wabunge wote kuvaa Barakoa appeared first on Bongo5.com.