Mpango wa siku tatu wa kusitisha mapigano umeanza kutekelezwa nchini Afghanstan, wakati waumini wa dini ya Kiislamu wakisherehekea sikukuu ya Eid al-Adha.

Kuna matumaini kwamba mapatano hayo ya muda na ubadilishanaji wafungwa vitapelekea kufanyika mazungumzo ya amani kati ya kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan. Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani aliamuru kuachiliwa huru kwa wafungwa wengine 50 wa Taliban mapema leo, wakati mpango huo wa usitishaji mapigano kwa masaa 72 ukianza.

Mapatano hayo yaliopendekezwa na Taliban na kukubaliwa na serikali mjini Kabul, yanatarajiwa kudumu kwa kipindi cha siku tatu za sherehe ya Eid al-Adha, na hatimaye kusafisha njia ya kufanyika kwa mazungumzo ya amani yaliosubiriwa kwa muda mrefu kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana.

Kusitishwa kwa mapigano na kubadilishana wafungwa - kulikojadiliwa katika makubaliano kati ya Taliban na Marekani mnamo mwezi Februari - ndiyo masharti ya kuanza kwa mazungumzo kati ya wa Afghanistan.