Mwanasiasa wa juu nchini Kenya ameomba radhi kwa kukiuka masharti ya kutotoka nje wakati wa usiku ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja alikutwa akinywa katika kilabu kimoja jijini Nairobi mwishoni mwa juma lililopita, saa kadhaa baada ya muda wa kutakiwa kuwa nyumbani kufika.
Alishikiliwa kwa muda mfupi katika kituo cha polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya polisi. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumanne lakini amesema yuko tayari kuwajibika kutokana na vitendo vyake.
Pia amejiondoa kwenye uongozi wa kamati ya seneti inayotazama mwenendo wa mapambano dhidi ya Covid-19.
Video ilisambaa mtandaoni siku ya Jumapili ikionesha seneta huyo akiwa akibishana na polisi baada ya kukamatwa.
Wakenya wamelalamika kuhusu hatua kali ambazo zimekuwa zikitekelezwa kwa ubaguzi, huku wanasiasa wakivunja sheria hizo kwa uwazi kabisa kwa kuitisha mikutano mikubwa ambayo imepigwa marufuku.
Polisi pia wamekosolewa kwa vitendo vya kuwapiga, kuwajeruhi na kuwaua Wakenya wakati wa kusimamia utekelezaji wa sharti la kutotoka nje.
Baadhi ya masharti makali kuhusu mikusanyiko ya kidini na marufuku ya kusafiri kutoka katika maeneo yenye maambukizi kwa kiasi kikubwa yaliondolewa ingawa idadi ya watu waliopata maambukizi ilikuwa ikiongezeka nchini humo.
Mpaka sasa Kenya imethibitisha kuwa na watu 13,000 walioambukizwa na vifo vya watu 234.
The post Seneta wa Nairobi akiuka masharti ya kutotoka nje kisa Corona, akutwa klabuni akinywa appeared first on Bongo5.com.