Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole , amesema viongozi wa umma wasioridhika na nyadhifa zao, hawana nafasi ndani ya chama hicho.

Polepole ametoa kauli hiyo jana Jumamosi tarehe 18 Julai 2020, wakati akizungumza katika mkutano wa kuelezea utekezaji wa Ilani ya CCM, katika Mkoa wa Ruvuma.

Licha ya kwamba Polepole hakuweka bayana viongozi hao wa umma hawaridhiki kivipi, katibu huyo wa uenezi amesema CCM inawasubiri kuwaona wakati wa uteuzi huku akiwapongeza viongozi wa kuteuliwa Mkoa wa Ruvuma kwa kutokuondoka.

Juzi Ijumaa saa 10 jioni, ndiyo ilikuwa mwisho wa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho katika nafasi za Ubunge, Udiwani na Uwakilishi.

Baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya, katibu tawala wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, mashirika ya umma pamoja na makatibu wakuu wameziacha nafasi zao na kwenda kugombea

 Kwa mujibu ya ratiba ya CCM, Tarehe 20 na 21 Julai 2020 itakuwa ni mikutano mkuu ya majimbo na wilaya kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge na ujumbe wa baraza la wawakishi.