Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesitisha kibali cha ndege za Kenya (KQ) kutua nchini rasmi kuanzia leo, Agosti 1.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Kenya kutoa orodha ya nchi ambazo raia wao wataruhusiwa kuingia nchini humo kwa ndege kuanzia leo watapofungua mipaka yao ya kimataifa.

Orodha hiyo haikuwataja Watanzania hivyo kupelekea Tanzania ambayo ilikuwa inaruhusu ndege za Kenya kuingia nchini kusitisha (nullify) ruhusa hiyo.

Ndege za Kenya hazitoruhusiwa kutua katika uwanja wa ndege wa JNIA – Dar es Salaam, KIA – Kilimanjaro, wala AAKIA – Zanzibar.

Kenya imetangaza kufungua anga lake kuanzia leo baada ya kulifunga kwa zaidi ya miezi minne ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.