MAMA mzazi wa msanii wa filamu nchini Wema Sepetu, Miriam Sepetu amefungukia ishu ya mwanaye kudaiwa kuanguka na kuzimia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, uvumi ulienea kwenye mitandao ya kijamii kuwa staa huyo wa filamu, alipatwa na hali hiyo akiwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar.“Hiyo juzi wanayoisema wao, mwanangu alizimia mimi nilikuwa naye kambini akimalizia kushuti tamthiliya yao season ya pili.
“Jana pia niliongea naye kwa muda mrefu sana na kama angekuwa amepatwa na hilo tatizo, angeniambia.
“Watu wameona mwanangu yupo bize sasa hivi na mambo yake, wameanza kumchokonoa,” alisema Miriam kwa ukali.Wachokonozi hao, anaowataja mama Wema, juzi kati waliposti kwenye mitandao ya kijamii kwamba staa huyo wa filamu, amekimbizwa hospitalini baada ya kupatwa na sintofahamu ya afya.

Ujumbe katika ukurasa mmoja wa Instagram (jina linatupwa) ulienda mbali zaidi na kudai si mara ya kwanza kwa Wema kuanguka na kupoteza fahamu na kudai kuwa amekuwa akipatwa na hali hiyo mara kwa mara.Inadaiwa kuwa, tangu apungue mwili, msanii huyo amekuwa na matatizo ya kiafya jambo ambalo Wema hajaweka wazi wakati wowote kukabiliwa na mgogoro wa afya yake.

“Jamani juzi Wema alizimia pale kwake na inavyosemekana, walimpeleka hospitali akaambiwa dawa alizotumia kupunguza mwili, sasa zimeanza kumzidi nguvu.

“Wanasema dawa hizo zimenyonya mafuta mengi mwilini, mpaka imekuwa hatari kwa afya yake,” mtu mmoja aliandika kwenye ukurasa wa Instagram.Ishu ya Wema kupungua mwili, ilikuwa gumzo miaka miwili iyopita ambapo upunguaji huo ulitajwa kutokana na upasuaji wa kukatwa utumbo, jambo ambalo mwenyewe amekuwa akilikanusha.

Mwandishi wetu alipomtafuta Wema ili kujua hayo ya mtandaoni anahusika nayo au ndiyo wabaya wanamzushia, hakuweza kupatikana baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.

Stori: Memorise Richard