Rais Magufuli amesema kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa matendo ambayo ameyatenda hasa katika kipindi kigumu cha ugonjwa wa Corona.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo wakati alipounganishwa kuzungumza Mubashara na tamasha la kumshukuru Mungu kwa matendo aliyoyatenda nchini.

“Siku ya leo imenilazimu kuja nikiwa na biblia tunakumbushwa kwenye kitabu cha Yeremea 33:3 ninaomba niusome nisije nikaukosea unasema hivi ” Niite nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa magumu usiyoyajua,”amesema Magufuli.

Aliongezea kuwa ” Sisi Watanzania tumemuita Mungu katika Mambo magumu ambayo tumeamini hatuwezi kuyashinda kwa nguvu zetu. Tumemuita Mungu katika kipindi cha Corona ni kipindi ambacho kilikuwa ni kigumu sana.. Mungu wetu mwema alisikia na akajibu majibu haraka sana,”

Magufuli amesema hata leo wanaposherehekea na kukusanyika kwa wote hakuna mtu ambaye anamuogopa mwenzake kwa sababu ya Corona.

“Shukurani kwa mwenyezi Mungu lakini pia Mungu huyo huyo amejumuika katika mambo mbalimbali ya nchi yetu. Tumeweza kuingia kwenye uchumi wa kati mapema sana kabla ya wakati ilikuwa ni kipindi kigumu katika nchi yetu lakini Mungu ametupigania,” amesema Magufuli.

Rais amesema katika tamasha hilo wamekusanyika watu mbalimbali katika dini lakini wameweza kukusanyika kwa jambo moja.

“Hicho ni kitendo ambacho naona ni cha ajabu kwa Watanzania ninawashukuru sana ndugu zangu viongozi ninawashukuru ninyi nyote mliokusanyika hapa kwa ajili ya jambo hili la kumshukuru Mungu kwa matendo makubwa. Mungu awabariki sana naona kwaya mbalimbali zimependeza kweli nilitamani na Mimi ningekuwa hapo baadaye nikawa namtafuta ndugu Polepole uko wapi angalau ufike tu uniwakilishe.. Asiende kuzungumza ya chama azungumze ya Mungu kwa sababu Mungu ni wa vyama vyote,” amesema Magufuli.

Aidha, Magufuli amesema wanaingia katika kipindi kingine cha uchaguzi ukasimamiwe vizuri na kumtanguliza Mungu uwe wa amani, tupendane na washikamane kwa ajili ya kujenga taifa.

“Mimi ninaamini katika siku zote tukiendelea kumtanguliza Mungu tutashinda. Ninawashukuru sana tumpe Mungu nguvu zake zote wanakwaya, wachungaji, wana Dar es Salaam ninawashukuru sana,” amesema Magufuli.