Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
kufuatia kupungua kwa maambukizi ya virusi vya COVID 19 Jeshi la Magereza nchini limefuta masharti ya katazo la huduma ya kuwatembelea wafungwa na mahabusu na huduma mbalimbali katika magereza ikiwamo huduma ya chakula kwa mahabusu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma msemaji wa Jeshi la Magereza SSP Amina Kavirondo amesema kutokana na serikali kuruhusu shughuri mbalimbali kuendelea Jeshi la Magereza limeondoa katazo hilo kuanzia Augusti 1, 2020.

''Jeshi la magereza limelegeza masharti ya katazo kuanzia 01/08/2020 huduma za kuwatembelea wafungwa na mahabusu kwa huduma mbalimbali magerezani zimerejeshwa'' amesema Amina.

Aidha jeshi la Magereza limewataka wageni wote pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya jeshi na Wizara ya Afya wakati wa upokeaji wa huduma hiyo wageni watatakiwa mambo ikiwamo mfungwa au mahabusu atatembelewa na ndugu wasiozidi wawili kwa siku za jumamosi na jumapili.

Pia limebainisha kuwa mazungumzo yatatakiwa kuto zidi dakika tano na wale wenye vibali vya kuleta chakula italazimika kuletwa na mtu mmoja tu, pia mgeni atatakiwa kukaa umbali wa mita moja kati ya mfungwa au mahabusu huku wakitakiwa kuvaa barakoa na kunawa kwa maji tiririka huku likibainisha kuwa mazungumzo ya kisheria kati ya wakili na mteja wake yasizidi saa moja.

Aidha amebainisha kuwa kwa kipindi ambacho jeshi liliweka katazo hilo wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya wafungwa kukosa haki zao ambazo zilikuwa zinahatarisha au kusababisha kusambaa kwa virus vya corona katika magereza lakini wamekuwa wakiwaelimisha lengo la kufanya hivyo.