KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael kwa mara kwanza ameamua kuvunja ukimya kwa kusema kuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mghana, Bernard Morrison amemsaliti na kuisaliti timu hiyo, naye hamtaki bora aondoke.
Morrison kwa sasa amekuwa akihusishwa na kujiunga na Simba baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika, hali inayopelekea kugoma kabisa kwenda mazoezi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Eymael amekiri kupokea lawama kutoka kwa watu wa Yanga kutokana na mchezaji huyo kuendelea kufanya matukio ya utovu wa nidhamu kwa kuwa yeye ndiye aliyemleta nchini kutokana na kujua ubora wake lakini hakutegemea kama angebadilika kitabia kama alivyo kwa sasa.
“Nimekuwa nikipokea lawama kutoka kwa watu Yanga juu ya Morrison kwa sababu ndiye niliyependekeza aletwe kwa kuwa najua kama ni mchezaji mzuri lakini sikutegemea wala kufi kiri kama angebadilika kitabia na kufanya haya ambayo ameyafanya.
“Morrison ukweli amekuwa msaliti kwangu mwenyewe, lakini amewasaliti wachezaji wenzake, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki ambao walikuwa wakimpenda ingawa haya yote yalitokea baada ya kupewa sifa asizostahili tangu aifunge Simba, nitawaambia viongozi wamuache aende anapotaka kwa kuwa sioni faida ya kuwa naye tena, nami simtaki,” alisema.