KOCHA wa zamani wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm ameibuka na kufungukia hatma yake ya kurejea kukinoa kikosi baada ya tetesi nyingi kuzagaa anakuja tena kwa mara ya tatu kuifundisha timu hiyo.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kocha huyo jina lake litajwe kwenye orodha ya makocha wanaowaniwa na Yanga baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mbelgiji, Luc Eymael kuachana naye.

Kocha mwingine anayetajwa ni Ernie Brandts naye raia wa Uholanzi ambaye jina lake linatajwa kwenye orodha ya makocha wanaotarajiwa kujiunga na Yanga katika msimu ujao.

Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema kuwa bado viongozi wa Yanga hawajamfuata kwa ajili ya kufanya mazungumzo, lakini yeye yupo tayari kurejea kukinoa kikosi hicho kama watahitaji huduma yake katika msimu ujao.

Pluijum alisema kuwa hivi sasa amewaachia viongozi wa Yanga ambao ndiyo watakaochukua maamuzi ya yeye kuja au kutokuja kukinoa kikosi hicho.

“Mashabiki wa Yanga wanaonekana kukumbuka ‘philosoph’ yangu ya uchezaji wa soka, hiyo ndiyo maana nimekuwa nikipokea meseji nyingi za kuniomba nirejee tena kuifundisha Yanga.

“Kwangu ngumu kusema ninakuja kuifundisha Yanga, kwani hayo ni maamuzi ya uongozi ambao kama utakuwa tayari kunirejesha, basi nitakuwa tayari kurejea tena.

“Kwa hivi sasa sina timu yoyote ninayoifundisha, hivyo kikubwa ni viongozi kunifuata na kufanya mazungumzo na mimi, kama tukifikia muafaka mzuri basi nitakuwa tayari kurudi, uzuri nawafahamu wachezaji baadhi ambao bado wapo niliwahi kufanya nao kazi, hivyo sitakuwa kazi kubwa,”alisema Pluijm.