INAELEZWA kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ tayari ameshamalizana na mabosi wa Azam FC kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na kinachosubiriwa ni kutambulishwa tu.

Kiungo huyo mara ya mwisho alionekana uwanjani akiwa na jezi ya Yanga katika mchezo dhidi ya Simba ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kabla ya kupotea kabisa kisha kuonekana tena akiwa katika maandalizi ya mchezo wa hatua ya nusu fainali Kombe la FA dhidi ya Simba ambao pia hakuweza kukaa hata katika benchi.

Taarifa zinaeleza kuwa tayari kiungo huyo ameshamalizana kila kitu na Azam FC, hali inayosababisha kutoweka ndani ya timu yake bila ya kuwepo kwa taarifa zozote.

“Mo Banka mbona ameshasaini mkataba na Azam muda mrefu, hawezi kubaki Yanga na ndiyo maana siku hizi hata mazoezini haonekani kabisa ndani yaYanga, Azam na mchezaji mwenyewe wanafanya siri hadi siku atakayotangazwa.

“Wamempa mkataba wa miaka miwili lakini hakuna atakayekuja kukubali katika kipindi hiki cha ligi ambayo haijaisha, jambo hilo ndilo limesababisha hata alivyokwenda Bukoba kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Simba mwalimu hakutaka kabisa kushughulika naye na baada ya kurejea ndiyo amesusa kabisa,” kilisema chanzo.


Kwa upande wa kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema kuwa hajui mchezaji huyo yupo wapi kwa sasa kwa kuwa hamuoni katika mazoezi kabla ya kuelekea mkoani Morogoro.

“Sasa hivi sijui chochote kuhusu Banka kwa sababu haji mazoezini, hivyo ni ngumu kuwa na taarifa zake hata meneja mwenyewe hajui yupo wapi ila tunachofanya ni kupambana kwenye mechi yetu iliyobakia kwa kutafuta matokeo mazuri,” alisema Eymael.