Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga August 5, mwaka huu kuanza kusikiliza jumla ya mashahidi 15 katika kesi inayomkabili Mchekeshaji Idris Sultan ya kushindwa kusajili laini ya simu iliyokuwa inamilikiwa na Mtu mwingine, mbali ya Idris, mshitakiwa mwingine ni Innocent Maiga.

Miongoni mwa mashtaka inadaiwa Mei 5, mwaka huu Mkuu wa Upelelezi Kinondoni alipewa taarifa kwamba Idris anatumia kadi ya simu ambayo haijasajiliwa kwa jina lake na kwamba alitakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay ambapo alifanya hivyo.

Inadawa Polisi walienda kufanya upekuzi nyumbani kwa Idris na kubaini uwepo wa laini hiyo ya simu na kwamba alikuwa akiitumia kwa mawasiliano yake ya kila siku licha ya kusajiliwa kwa jina la Maiga.

Upande wa mashitaka umedai wataleta mashahidi 15 na kama watahitaji kuongeza au kupunguza mashahidi wataieleza Mahakama na kwamba wataeleza idadi ya vielelezo watakavyokuwa navyo kesi itakapoendelea.