Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa DSM Paul makonda amewashukuru wale wote waliompa pole nyingi baada ya matokeo ya jana aliyoyapata kwenye kura za maoni Jimbo la Kigamboni na kusema kuwa jambo moja muhimu ni kuyajua mapenzi ya Mungu.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 21, 2020, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram na kuongeza kuwa anayo imani kuwa mapenzi ya Mungu katika jambo hilo ni makubwa kuliko hata mapenzi yake, huku akiwashukuru wana Kigamboni kwa upendo wao.

"Nimepata pole nyingi sana kutokana na Matokeo ya jana, kwanza nawashukuru kwa upendo wenu na maombi yenu ya kunitakia mafanikio katika kutimiza ndoto yangu, jambo moja kubwa na muhimu ni kuyajua mapenzi ya Mungu na katika hili mapenzi ya Mungu ni makubwa kuliko mapenzi yangu, nawatakia baraka na afya njema siku zote za maisha yenu, asanteni sana sana wana Kigamboni kwa upendo wenu na kunipa nafasi niwe sehemu ya maisha yenu" ameandika Makonda.

Jana katika zoezi la uchaguzi wa kura za maoni Jimbo la Kigamboni, Makonda alipata kura 122, ambapo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Dkt Faustine Ndugulile akiongoza kwa kupata kura 190.